Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu vikali matamshi ya Rais Joseph Aoun wa Lebanon dhidi ya Iran, akiweka wazi kuwa kiongozi huyo anashindwa kutofautisha kati ya marafiki na maadui wa nchi yake.

“Anamuuza anayesimama pamoja naye, na kumnunua anayempinga. Humtelekeza aliyemuunga mkono, na kuwa pamoja na anayemkaba,” Ismail Baqaei aliandika maneno haya kwa lugha Kiarabu kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X jana Jumamosi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia aliutuma tena ujumbe wa Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ambapo mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu alikosoa matamshi ya Rais Aoun wa Lebanon.

Katika mahojiano yake na Christiane Amanpour wa CNN Rais wa Lebanon ameituhumu Iran kuwa inaitumia Lebanon kama “wenzo wa kujinufaisha” katika mazungumzo na Marekani kwa lengo la kufikia makubaliano ya kuhitimisha vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran mwishoni mwa Februari.

Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alimjibu Rais wa Lebanon kwa kusema: “Lau Lebanon ingekuwa wenzo wa manufaa kwa Iran katika mazungumzo, tungefikia makubaliano muda mrefu uliopita.” Araqchi amemtaka Rais Aoun azingatie “adui halisi” wa Lebanon badala ya Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza zaidi kwamba maoni ya Aoun yamepuuza tishio kuu linaloikabili Lebanon na kueleza isivyo chanzo cha changamoto za sasa za nchi hiyo.

Rais wa Lebanon ametoa kauli hiyo dhidi ya Iran huku Tehran ikisisitiza kuwa makubaliano yoyote ya kuhitimisha vita lazima yajumishe suala la kukomesha mapigano katika medani zote hasa huko Lebanon ambako harakati ya Hizbullah inapigana dhidi ya Israel tangu mwezi Machi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *