Balozi wa Iran: BRICS ina jukumu muhimu katika usalama wa nishati duniani

Kazem Jalali aliyasema hayo jana Jumamosi kwenye mkutano wa “Mtazamo wa Maendeleo wa BRICS: Mabadiliko na Upeo Mpya” uliofanyika pambizoni mwa Kongamano la 29 la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg.

“Mvutano wa kijiografia na kisiasa, kuvurugwa minyororo ya ugavi, kuwepo mabadiliko katika soko la kimataifa, na kuongezeka mahitaji katika nchi zinazoinukia kiuchumi kunaonyesha kwamba usalama wa nishati umekuwa nguzo kuu ya utulivu wa kimataifa, na maendeleo kuliko hapo awali,” amesema Balozi Jalali alipokuwa akifafanua maoni ya Jamhuri ya Kiislamu kuhusu nafasi ya BRICS katika mfumo wa nishati duniani.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran aliendelea kusema: Usalama wa nishati haimaanishi tu upatikanaji wa rasilimali za nishati, lakini ni dhana pana ambayo pia inajumuisha usalama wa usambazaji, usalama wa mahitaji, usalama wa uwekezaji, usalama wa teknolojia, usalama wa miundombinu na wa kifedha.

Balozi wa Iran nchini Russia pia amesisitiza kuhusu uwezo mkubwa wa nchi wanachama wa BRICS wa kusimamia majukumu ya pamoja.

Amesema, nchi wanachama wa BRICS zina jukumu la kutoa mchango ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo mfumo wa haki, madhubuti na jumuishi zaidi kwa ajili ya usalama wa nishati duniani.

Aidha amesisitiza kuwa nishati inapasa kuwa kigezo cha maendeleo, ustawi na uzalishaji na si wenzo wa mashinikizo ya kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *