Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametangaza kwamba wafanyakazi 136 wa shirika hilo la kimataifa waliuawa wakitekeleza majukumu yao katika mwaka uliopita, wakiwemo wafanyakazi 80 waliokuwa wakifanya kazi katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Guterres alisema wakati wa shughuli ya kuwakumbuka wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliofariki dunia mwaka jana kwamba waathiriwa walitoka nchi 32, wakiwemo wafanyakazi wa kiraia 97 na walinda amani 39.

Ameeleza kuwa 80 kati ya waliouawa walikuwa wakifanya kazi kwenye Shirika la Misaada na Kazi la Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) katika Ukanda wa Gaza.

Guterres amefichua kwamba idadi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliouawa huko Gaza imezidi idadi ya wafanyakazi ambao shirika hilo lilipoteza katika mzozo au maafa mengine yote katika historia yake.

Ameongeza kuwa baadhi ya wafanyakazi waliuawa pamoja na wanafamilia wao katika nyumba zao au maeneo ya kukimbilia, huku wengine wakiuawa walipokuwa wakitekeleza majukumu yao katika ofisi, makazi na jamii walizokuwa wakihudumia.

Guterres amesisitiza kwamba kuwalenga wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, walinda amani na wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Licha ya kuthibitika kuwa Israel ilihusika katika mauaji ya wafanyakazi hao wa Umoja wa Mataifa lakini hadi sasa jamii ya kimataifa haijachukua hatua yoyote ya maana ya kuuwajibisha utawala huo katili kwa kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko katika Ukanada wa Gaza.  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *