
BEKI wa Yanga, Chadrack Boka yupo kwenye presha ya kusalia katika kikosi hicho baada ya mabosi wa klabu hiyo kuanza hesabu za kusaka kwa mabeki wawili wa kigeni wa kuchukua nafasi yake.
Mkataba wa Boka na Yanga unafikia tamati katikati ya msimu ujao, akibakiza miezi sita na mabingwa hao ambapo awali alisaini miaka miwili na nusu akitokea FC Lupopo ya DR Congo, lakini kiwango chake kinawapa shida mabingwa hao.
Yanga inataka beki imara zaidi ya Boka ambaye atakuwa na ubora wa kuzuia, lakini ikitaka mtu ambaye atakuwa na umaliziaji mzuri wa krosi zake au pasi za mwisho, kitu ambacho beki huyo Mkongomani anaonekana kukishindwa.
Msimu huu Boka licha ya kucheza jumla ya michezo 25 kwenye mashindano tofauti, lakini hajafanikiwa kufunga bao lolote wala kutengeneza asisti, takwimu ambazo zimekuwa zikimtibulia beki huyo wakati mwenzake Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akiwa na asiti moja na mabao mawili.
Yanga inatafuta beki wa maana zaidi ikitaka kuboresha eneo hilo na msako huo unamlenga Boka kutokana na kuegemea kwenye wachezaji wa kigeni na sasa kuna majina mawili ambayo yanaendelewa kufanyiwa kazi.
Chaguo la kwanza kwa Yanga ni beki wa kushoto raia wa Uganda, Aziz Kayondo ambaye kwasasa anacheza soka nchini Czech akiitumikia klabu ya Liberec kwa mkopo akitokea MFK Vyskov ya hapo hapo.
Kama ambavyo Yanga inapata shida na Boka na Liberec ambayo haina matokeo mazuri ikipoteza mechi zake tano za mwisho licha ya Kayondo kukosa mechi moja tu kati ya tano za mwisho, lakini nao wanatamani kuwa beki imara zaidi anayeweza kuzalisha mabao au kutoa asisti.
Mabosi wa Yanga wamepenyezewa taarifa kwamba Kayondo yuko tayari kurudi Afrika lakini pande hizo mbili zinashindana kwenye maslahi binafsi kati ya klabu hiyo na beki huyo anayejua kupandisha mashambulizi.
“Chaguo letu la kwanza ni yule Kayondo (Aziz )kuna eneo tunashindana, juu ya maslahi, lakini amekubali kurudi Afrika, bado tunazungumza naye hatujakata tamaa, jambo zuri amejiridhisha kwamba Yanga ni klabu sahihi kwake,” alisema bosi huyo. “Kayondo anaamini anaweza kuja Yanga na akaendelea kuitwa timu ya taifa akiona kaka yake Aucho (Khalid) na hata Okello (Allan) naye amekuja sasa hapa na ameendelea kutunza nafasi yake kwenye timu ya taifa.
Mbali na Kayondo, Yanga pia imefanya mazungumzo na beki Samba Kone anayeichezea FC Mouna ya Ivory Coast, aliyesajiliwa na klabu hiyo deirisha la Januari akitokea Paradou AC ya Algeria.
Kone amefanikiwa kurudisha kiwango chake baada ya kutengeneza asisti nne kwenye mechi za ligi, pia mbili zingine akitengeneza kwenye kombe la taifa, Yanga ikimfanya kuwa chaguo lao la pili.
“Chaguo letu la pili ni Kone yupo Ivory Coasta huyu sio shida kumpata kila kitu kipo sawa tunachotaka kwanza ni kupata uhakika wa Kayondo, kama tukishindwa kwa Kayondo tutamalizana naye,anatamani kuja hapa.
Yanga imetoa msimamo Tshabalala ataendelea kusalia ambapo licha ya kukosa kucheza kwenye mechi tano na moja akiwa benchi kutokana na majeraha, lakini mkongwe huyo aamehakikishiwa kusalia kwenye kikosi hicho.
“Tshabalala atabaki hilo halina mjadala, huyu ni mchezaji wa ndani lakini mwaka wake wa kwanza hapa ameonyesha hatukukosea kumsajili, ni haya majeraha tu, lakini yupo sawasawa tunachofanya sasa ni kutafuta mtu bora ambaye watashirikiana eneo lake.”