Marekani yashambulia kigaidi kituo cha maji ya kunywa Hormozgan, Iran

Abdolhamid Hamzehpour aliwaambia waandishi habari siku ya Jumatano kuwa mashambulizi ya kigaidi ya Marekani yalilenga vituo vya usambazaji maji katika kaunti ya Sirik, yakiharibu mtandao wa usambazaji kwa mji wa Kuhestak na vijiji 10 vya wilaya ya Bemani.

Hamzehpour amesema kuwa hifadhi mbili za maji zenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 500 na 2,000, pamoja na vifaa vyake vya kimitambo, ziliharibiwa kabisa katika mashambulizi hayo. Uharibifu huo umesababisha kusitishwa kabisa kwa usambazaji maji katika maeneo yaliyoathiriwa.

Amesema, “Adui amelenga kwa makusudi miundombinu inayohusiana moja kwa moja na maisha ya kila siku na afya ya wananchi,” akielezea kitendo hicho kama “ugaidi wa wazi.”

Kukatika kwa maji kumetokea wakati eneo hilo linakabiliwa na kilele cha joto, huku taarifa zikionyesha kuwa halijoto inafikia kati ya nyuzi joto 45 hadi 50 za Selsiasi. Maafisa wamesema kuwa eneo hilo halina akiba ya kutosha ya maji ya chini ya ardhi kufidia upotevu wa hifadhi hizo, jambo linalozidisha hali ya dharura kwa wakazi.

Hamzehpour amelaani kulengwa kwa huduma ya maji kama “mfano dhahiri wa uhalifu dhidi ya ubinadamu,” akibainisha kuwa timu za kiufundi ziko eneo la tukio lakini zinakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na ukubwa wa uharibifu.

Mashambulizi dhidi ya Sirik, pamoja na miji ya Jask na Kisiwa cha Qeshm katika Mlango wa Hormuz, yalifanyika usiku wa kuamkia Jumatano. Hujuma hiyo ilifuatia madai ya Washington kwamba eti Iran iliangusha helikopta ya kijeshi ya Marekani aina ya Apache katika maji ya Ghuba ya Uajemi.

Ingawa Marekani imesema kuwa mashambulizi yake yalilenga miundombinu ya kijeshi, ikiwemo mifumo ya ulinzi wa anga na mitambo ya rada karibu na Mlango wa Hormuz, maafisa wa mkoa wa Iran wanasisitiza kuwa vituo vya maji vya kiraia huko Sirik vililengwa moja kwa moja.

Katika kujibu vitendo hivyo vya uchokozi, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilianzisha msururu wa mashambulizi ya droni na makombora dhidi ya mali za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.

Katika tukio moja, IRGC ililenga Kikosi cha Tano cha Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa mashambulizi ya makombora na droni, kama sehemu ya kampeni pana ya kulipiza kisasi.

Vikosi vya ulinzi vya Iran vilifanya mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Jordan, Bahrain na Kuwait katika saa za mapema za Jumatano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *