Gazeti mashuhuri la The New York Times limesema kuwa mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya miundombinu ya maji kusini mwa Iran yanaweza kuhesabika kama uhalifu wa kivita, kwani kulenga miundombinu ya kiraia ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa.

Mapema Jumatano, Kamandi Kuu ya Kijeshi ya Marekani (CENTCOM) ilitangaza kupitia mtandao wa X kuwa imetekeleza mashambulizi karibu na Mlango Bahari wa Hormuz “kwa kutumia zana za usahihi wa hali ya juu kutoka kwa ndege za kivita za Jeshi la Anga na Wanamaji la Marekani.”

Hata hivyo, maafisa wa eneo hilo nchini Iran wametangaza kuwa mashambulizi hayo ya Marekani yalipiga matanki mawili makubwa ya kuhifadhia maji huko Bamani, kusini mwa Iran. Afisa mmoja wa eneo hilo alibainisha kuwa huduma ya maji kwa zaidi ya watu 20,000 katika mji huo na vijiji vya jirani imekatika kabisa.

Uchambuzi uliofanywa na gazeti la The New York Times kupitia picha za satelaiti na video zilizotolewa na mamlaka za mkoa ulihitimisha kuwa kitendo cha Marekani kulenga miundombinu hiyo ya maji kinaweza kuhesabiwa kuwa ni uhalifu wa kivita.

Gazeti hilo lilieleza: “Kulenga kimakusudi miundombinu ya kiraia kunaweza kuunda mazingira ya uhalifu wa kivita.”

Tangu kuanza kwa vita vya uchokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28, vikosi vya Marekani vimetekeleza vitendo vingi ambavyo wataalamu wa sheria na mashirika ya haki za kibinadamu wamevilaani kama uhalifu wa kivita.

Katika siku ya kwanza ya vita hivyo, kombora la Marekani la Tomahawk lilipiga shule ya msingi ya Shajareh Tayyebeh katika mji wa kusini wa Minab wakati wa masaa ya masomo. Shambulio hilo liliua watu 168, wengi wao wakiwa ni wanafunzi. Shambulio hilo limetajwa kuwa kitendo cha makusudi cha “ugaidi” kilicholenga kuwatisha na kuwatia woga raia wa Iran.

Aidha, mashambulizi ya Marekani na Israel yamekuwa yakipiga hospitali na vituo vya matibabu mara kwa mara kote nchini Iran. Hospitali ya Gandhi mjini Tehran iliharibiwa vibaya, huku kitengo chake cha uzazi cha IVF kikiharibiwa kabisa.

Taasisi ya Pasteur ya Iran, ambayo ni taasisi ya afya ya umma ilianzishwa miaka 106 iliyopita, nayo ilipigwa kwa mabomu na kulazimika kusitisha huduma zake, jambo lililovuruga uwezo wa nchi kufuatilia magonjwa na kuzalisha chanjo.

Mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel pia yamelenga makazi ya raia katika miji kadhaa ya Iran, na kuua mamia ya raia. Nyumba ya ibada ya Kiyahudi (Sinagogi) mjini Tehran nayo ilipigwa kwa mabomu, kitendo ambacho mwakilishi wa jamii ya Kiyahudi nchini Iran alikilaani akisema ni thibitisho la “chuki ya kupita kiasi” ya Israel dhidi ya Wayahudi wa Iran.

Vikosi vya Marekani pia vimeshambulia miundombinu mingine ya kiraia ikiwemo vituo vya kuzalisha umeme, madaraja, viwanda vya kusafisha mafuta, na eneo la gesi la South Pars, ambalo ni uwanja mkubwa zaidi wa gesi asilia duniani. Mashambulizi haya yaliesababisha kukatika kwa umeme, uhaba wa mafuta, na uharibifu wa mazingira unaoathiri mamilioni ya raia.

Licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Pakistan tangu mapema mwezi Aprili, Marekani imeendeleza kizuizi haramu dhidi ya bandari za Iran. Wataalamu wa sheria za kimataifa wanasema hatua hiyo yenyewe ni kitendo cha uchokozi chini ya Azimio Nambari 3314 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Maafisa wa Iran wameapa kuendelea kuweka kumbukumbu za uhalifu huo wa kivita wa Marekani na kuchukua hatua za kisheria katika taasisi na mahakama za kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *