
Ripoti ya Newsweek inaonyesha kwamba kutimiza umri wa miaka 80 Rais wa Marekani Donald Trump kumerejesha mjadala wa umri na afya ya rais katika mstari wa mbele wa malumbano ya kisiasa nchini Marekani, baada ya yeye mwenyewe kufanya umri na utimamu wa akili wa mtangulizi wake, Joe Biden kuwa moja ya mada kuu za kampeni yake ya uchaguzi.
Jumapili hii Trump alisherehekea mwaka wa 80 wa kuzaliwa kwake, na kuwa rais wa pili wa Marekani kufikia umri huo akiwa madarakani baada ya Joe Biden. Pia anatarajiwa kuondoka Ikulu ya White House mwishoni mwa muhula wake wa pili kama rais mzee zaidi katika historia ya Marekani.
Jarida hilo linaeleza kuwa utata huo hauhusiani na umri wa Trump pekee, bali uwazi kuhusu afya yake na ripoti za matibabu zimekuwa suala la kisiasa lenye taathira kubwa huku uchaguzi wa katikati ya muhula ukikaribia huko Marekani mwezi Novemba mwaka huu.
Trump amejaribu mara kwa mara kuondoa wasiwasi kuhusu umri na uwezo wake wa kimwili na kiakili, akisisitiza katika mahojiano Februari mwaka huu kwamba anajihisi kimwili na kiakili kama alivyokuwa akihisi miaka hamsini iliyopita.
Japokuwa tabibu wa rais huyo wa Marekani anasema kuwa Trump ana afya nzuri na kwamba ana uwezo wa kusimamia majukumu yake kama Amiri Jeshi Mkuu, hata hivyo gazeti hilo linabainisha kwamba baadhi ya wataalamu hutazama ripoti hizo kwa tahadhari kwa sababu ya kile kilichoelezwa kama kutia chumvi kwa hapo awali katika kuelezea hali ya afya ya rais, pamoja na taarifa chache zilizotolewa na mamkala husika kuhusu rekodi yake ya matibabu.
Katika muktadha huu, S.J. Olshansky, mtafiti wa afya ya umma katika Chuo Kikuu cha Illinois huko Chicago, ametaka rekodi kamili ya matibabu ya rais wa Marekani ichapishwe bila kukatwakatwa, akisema kwamba hii itakuwa njia bora ya kumaliza utata unaohusu afya yake.
Ripoti hiyo inasisitiza kwamba Trump sasa anakabiliwa na kitendawili cha kisiasa, kwani mashambulizi yake makali dhidi ya Biden chini ya kauli mbiu “Sleepy Joe” (Joe Biden anayesinzia ovyo) yamefanya suala la umri wake kuwa na umuhimu zaidi katika tathmini ya wapiga kura kuhusu marais.
Wakati huo huo, kura za maoni zinaunga mkono mwelekeo huu; kura za maoni za Januari zilionyesha kuwa karibu nusu ya Wamarekani wanaamini Trump ni mzee sana kuwa rais, huku kura nyingine za maoni za Reuters/Ipsos mwezi Februari zikionyesha kuwa 61% ya Wamarekani wanaamini kuwa ni mzee sana kuweza kutekeleza majukumu ya urais.