
Baada ya takriban mwezi mmoja wa uchunguzi rasmi, Paris imeituhumu kampuni ya Israel kwa kuingilia uchaguzi uliopita nchini Ufaransa, na imetaka maelezo kutoka Tel Aviv kuhusu suala hilo.
Tuhuma hizo za Ufaransa dhidi ya kampuni ya Israel inayojulikana kama ” BlackCore” hazikuhusu tu kuingilia kati kwake katika uchaguzi wa Ufaransa, bali zilienea hadi kwenye ushawishi wa kampuni hiyo katika matukio ya kisiasa kwenye nchi zingine kama vile Angola, Togo na Scotland, pamoja na uchaguzi wa manispaa katika Jiji la New York, Marekani mwaka wa 2025.
Alkhamisi iliyopita, Marc-Antoine Brillant, mkuu wa Shirika la Kitaifa la Ufaransa la Kufuatilia na Kupambana na Uingiliaji Kati wa Kidijitali na Taarifa Potofu, alitangaza katika mkutano na waandishi wa habari na Waziri Mkuu Sebastien Lecornu maelezo kuhusu hujuma ya kampuni ya Israel dhidi ya chama cha France Unbowed, (LFI) ambacho kinaunga mkono haki za watu wa Palestina.
Uchunguzi uliofuatilia jiografia ya chombo cha kigeni kilicho nyuma ya kampeni ya uingiliaji kati huo umefichua uhusiano na kampuni inayoshukiwa kujihusisha na ushawishi wa kidijitali inayoitwa “BlackCore” yenye makao yake makuu huko Israel. Marc-Antoine Brillant amesema kwamba wachunguzi bado wanafuatilia mfadhili wa uingiliaji kati huo katika uchaguzi na masuala ya ndani ya Ufaransa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu Agency, kampuni hiyo ya Israel iliingilia uchaguzi wa manispaa ya Ufaransa, ikiwa ni pamoja na kashfa za kidijitali na kampeni za kashfa dhidi ya wagombea watatu wa vyama vya siasa kabla ya uchaguzi wa manispaa uliofanyika Machi mwaka huu.
Kama ilivyo kwa chama cha mrengo wa kushoto cha Ufaransa, vyama vingine vya kisiasa vilivyolengwa na kampuni hiyo ya Israel vinawasilisha mjadala wa kimataifa unaounga mkono haki za watu wa Palestina na kupinga uvamizi wa Israel.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari wakati huo, kampeni hiyo ilijumuisha uundaji wa tovuti za kupotosha maoni ya umma na akaunti bandia za mitandao ya kijamii zilizoeneza madai ya tuhuma za tabia za uhalifu dhidi ya wagombea wenye misimamo ya kuwatetea Wapalestina na mapambabno yao ya kupigania uhuru.
Brillant hakutaja waziwazi ni nani aliyelengwa na kampuni hiyo ya Israel katika uchaguzi wa Jiji la New York mwaka jana, ambako Zohran Mamdani, meya wa kwanza Mwislamu wa jiji hilo aliibuka na ushinda. Mamdani alitetea haki za Wapalestina na kukosoa “mauaji ya kimbari” ya Israel huko Gaza.