
Waziri Mkuu wa Uingereza jana alisema nchi hiyo itapiga marufuku watoto walio na umri wa chini ya miaka 16 kutumia programu mbalimbali za mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Snapchat, TikTok na YouTube ili kuwalinda vijana dhidi ya maudhui hatari na kupoteza muda mwingi katika mitandao ya kijamii.
Keir Starmer amesema katika mkutano wa wanahabari kwamba atafanya kila awezalo ikiwa kampuni za teknolojia zitapinga hatua hiyo. Aidha amekiri kuwa baadhi ya vijana watajaribu kutafuta njia nyngine ya kuingia kwenye mitandao ya kijamii lakini amesema “hayuko tayari kuhatarisha usalama watoto wao.”
“Kila mzazi anaweza kuona kwa macho yake mwenyewe. Mitandao ya kijamii inawakosesha furaha watoto,” amesema Starmer ambaye ana watoto wawili barobaro.
“Nimesikia moja kwa moja kutoka kwa familia mbalimbali zikitaka kufanyike mabadiliko; nasi tutafawanyia kilicho sahihi,” ameongeza Waziri Mkuu wa Uingereza.
Hatua hiyo, inayotarajiwa kutekelezwa mapema mwaka ujao, inaifanya Uingereza kuwa sehemu ya harakati zinazokua za kimataifa za kuimarisha usalama mtandaoni kwa watoto. Australia, Canada, Brazil na Indonesia zimeanzisha sheria au kutangaza vizuizi vya umri au mahitaji ya ufikiaji wa watoto kwenye mitandao ya kijamii.
Nazo Ufaransa, Uhispania, Denmark, Thailand na Korea Kusini ni kati ya nchi nyingine zinachunguza au kuchukua hatua sawa na ya Uingereza.
Uingereza inapanga kufuata mtindo sawa na wa Australia wa marufuku ya mitandao ya kijamii, ambayo mwaka jana ilikuwa nchi ya kwanza kuwazuia watoto wenye chini ya miaka 16 kumiliki akaunti za mitandao ya kijamii. Majukwaa ambayo yameshindwa kuchukua hatua zinazofaa kuwaweka watoto walio na umri wa chini ya miaka 16 mbali na mitandao ya kijamii yanaweza kuadhibiwa kwa faini ya mamilioni ya dola.