
Kutoka ndani ya hospitali hizo mjini Gaza zilizoharibiwa na vita, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF James Elder kwa njia ya video ameelezea hali aliyoshuhudia mwenyewe. Anasimulia njisi msichana mdogo wa miaka sita, Aya, aliyeokolewa kutoka chini ya kifusi, alivyoaga dunia mbele ya macho yake huku madaktari wakijaribu kumwokoa bila mafanikio.
“Nilipoingia, ilikuwa ni kama uwanja wa vita watoto wamelala sakafuni, kuna kijana aliyepigwa risasi akivuja damu. Kila upande wa shoroba umejaa wagonjwa.”
Elder ameongeza kuwa hata watoto wachanga njiti waliozaliwa kabla ya wakati wanapigania uhai wao. Anasema alikutana na watoto watatu wakishirikiana mtungi mmoja wa hewa ya oksijeni kila mmoja akipumua kwa dakika ishirini pekee kabla ya bomba kumpa mwingine, huku wawili wengine wakilia kwa uchungu.
Kutoka Shirika la Afya la Umoja wa Mataiifa Duniani WHO, Dkt. Rik Peeperkorn mwakilishi wa shirika hilo katika Ukanda wa Gaza amesema hofu imetanda kila kona ya Gaza. “Watu wanaogopa. Watu wanaogopa, na kwa haki kabisa. Yaani kila mtu. Nimekuwa kwenye operesheni nyingi, na kila mtu anaogopa.”
Na hofu hiyo imezambaa Gaza nzima. Kwa upande wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC msemaji mkuu Christophe Cardon ameonya kuwa hospitali sasa si salama tena, kwani hata wodi zinaingiliwa na risasi.
“Hivi karibuni kabisa, risasi zilizovurumishwa hovyo zimewaweka hatarini wagonjwa na wale wanaofanya kazi hospitalini. Tumeshuhudia matukio kadhaa ambapo watu waliletewa hospitalini wakiwa wamejeruhiwa, na walipokuwa wakipokea matibabu, wakaumizwa tena kwa sababu ya risasi zilizopenya na kuingia hospitalini.”
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema mashambulizi ya kijeshi ya Israel yanayoendelea Jijini Gaza yamewanasa makumi ya maelfu ya raia, wakiwemo kina mama na watoto wao wachanga, watoto waliopoteza viungo, na familia zinazotafuta chakula cha msingi kama mkate.
Wametaka kulindwa kwa raia, kuachiliwa kwa upatikanaji wa msaada, na kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Kwa sasa, Umoja wa Mataifa unasema hospitali za Gaza zimegeuka kuwa uwanja wa mapambano, ambapo watoto na wagonjwa ndio wanaobeba gharama kubwa zaidi ya vita hivi visivyo na kikomo.