BAADA ya kuchukua pointi tatu jijini Mbeya dhidi ya Mbeya City, Simba imesema kwa sasa akili na nguvu zipo katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (CRDB) dhidi ya Coastal Union, ikisisitiza kuwa inahitaji ubingwa wa michuano hiyo.
Mechi kati ya Simba dhidi ya Coastal ambayo itakuwa ya kwanza kabla ya Yanga kuvaana na Azam itapigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid leo.
Hata hivyo, Coastal Union imesema isichukuliwe kinyonge kwani kufika kwao hatua hiyo si bahati mbaya badala yake wamejipanga kuhakikisha wanaweka historia ya kubeba ubingwa wa kombe hilo.
Simba ilitinga nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuitandika mabao 4-0 TRA United, ilhali Coastal Union wakifuzu kufuatia ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Singida Black Stars baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Utamu wa mchezo huo ni wa kuendeleza rekodi au kulipa kisasi kutokana na wapinzani kukutana mara ya mbili msimu huu, huku Simba ikijivunia ushindi mmoja na sare mchezo mmoja.
Kama Coastal Union itafuzu hii itakuwa si mara ya kwanza kucheza fainali ya michuano hiyo kama ilivyo Simba, ambapo mara ya mwisho ilifanya hivyo, mwaka 2022 ilipokutana na Yanga hapo hapo jijini Arusha na kupoteza kwa penalti 4-1 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 3-3.
Kwa upande wa Simba yenyewe imeshatwaa ubingwa huo mara sita na mara yao ya mwisho kuchukua ubingwa huo ilikuwa msimu wa 2020–21 ilipochukua ubingwa huo kwa kuichapa Yanga.
Akizungumza Kocha Mkuu wa Simba Steve Barker amesema kwa sasa ligi ni ngumu lakini anachofurahi ni kuona wachezaji wake wanapambana kupata pointi tatu, matokeo yanayotoa matumaini katika kufikia malengo yao.
Amesema kwa sasa akili na nguvu zao zinaelekezwa kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (CRDB) akitoa matumaini kuwa wamejipanga kufanya vizuri na kiu yao ni kufika fainali na kulisaka kombe.
“Niwapongeze na kuwashukuru wachezaji kwa namna wanavyopambana kia mchezo kupata pointi tatu, tumekuwa na ratiba ngumu ambayo tunapaswa kukabiliana nayo.”
“Tunaelekeza nguvu zetu kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union kuhakikisha tunashinda na kufuzu fainali na kuianza kampeni yetu ya kutafuta ubingwa wa michuano hiyo, tunajua mchezo hautakuwa rahisi ila tutapambana,” amesema Barker.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias amesema hawajafuzu hatua ya nusu fainali kwa bahati mbaya badala yake wanayo malengo na wamekusudia kufanya vizuri katika michuano hiyo.
Amekiri kuwa wanafahamu mchezo hautakuwa mwepesi kutokana na malengo ya kila timu, akibainisha kuwa watawaheshimu wapinzani kuhakikisha wanafikia ndoto zao za kutwaa ubingwa.
“Tumeshafika Arusha, pigo moja ni kumkosa nyota wetu Bakari Msimu lakini yupo mbadala wake, tunaiheshimu Simba na sisi lengo letu ni kurejea kwenye historia yetu ya kucheza fainali lakini tukilenga kuvuka na kuandika rekodi ya ubingwa”
“Hatutacheza kulipa kisasi kwakuwa ni mechi za mashindano mawili tofauti, wanaotubeza kwamba tumefuzu kwa bahati wasubiri kuona, tuko imara na tumedhamiria kufanya makubwa,” amesema.
Baada ya mchezo huo, kesho Yanga itakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kuvaana na Azam kwenye nusu fainali nyingine.