MIRADI YENYE GHARAMA YA BILIONI 2.8 KUTEMBELEWA NA MWENGE MKINGA

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga Mheshimiwa Gilbert Kalima ametoa wito kwa Wananchi wa Wilaya hiyo kushiriki kuupokea Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ambapo Mwenge huo utapokelewa Juni 22, 2026 ukitokea Wilaya ya Tanga ambapo mapokezi rasmi yatakafanyika katika Shule ya Msingi Mtimbwani, Kata ya Mtimbwani.

Aidha, Mwenge wa Uhuru utatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.8 ambapo ni pamoja na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi minne ikiwemo miwili ya elimu, jengo la OPD na mradi wa uchakataji wa mazao ya Mkonge sambamba na kuzindua mradi mmoja wa maji utakaosaidia kukabili adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, na kukagua mradi wa Kikundi cha Vijana wanaolima Mwani.

Mhe. Kalima ametoa wito kwa Wananchi wote wa Wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kuupokea, kuukimbiza na kukesha na Mwenge wa Uhuru ambapo mkesha utafanyika katika Kijiji cha Maforoni kwakuwa mwongozo wa mwaka huu umebainisha ya kwamba Mwenge ni Wananchi hivyo watapewa Kipaumbele kuukimbiza Mwenge wa Uhuru.

“Mwongozo wa Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu unaelekeza ya kuwa Mwenge ni Wananchi na wao ndio watapewa Kipaumbele kuukimbiza, si kama miaka ya nyuma ya kwamba ulikuwa ukikimbizwa kwenye magari tu kwa hivyo nawahimiza Wananchi wote wa Wilaya ya Mkinga mje kwa wingi wakati wa mapokezi na katika miradi yote iliyoandaliwa kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru”. Alieleza DC Kalima.

Kwa upande mwingine amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 2.8 kimetokewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo muhimu.

Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”

Mkuu wa Wilaya amezisisitiza taasisi zote za Serikali, binafsi pamoja na Wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki kuukimbiza Mwenge wa Uhuru.

#StarTvUpdate

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *