Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaambia wavamizi wa Kizayuni kwamba ikiwa hawataondoka kusini mwa Lebanon kwa miguu yao wenyewe, watafukuzwa kwa fedheha hali ya kuwa wameshindwa.

Brigedia Jenerali Esmail Qaani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameandika kwenye ukurasa wake binafsi wa mitandao ya kijamii kwamba: “Wavamizi na magaidi wa Kizayuni, mmeua watu 100 katika kipindi cha chini ya siku 4!!! Msipoondoka kusini mwa Lebanon kwa miguu yenu wenyewe, tukio kuu la mwaka wa 2000 litakaririwa; mwaka uleule mliokimbia kusini mwa Lebanon kwa madhila.”

Qaani ameongeza kuwa: “Ikiwa mtaendeleza uchokozi na uvamizi, mtafukuzwa kwa fedheha na kushindwa.”

Ujumbe huo wa Brigedia Jenerali Esmail Qaani umefuatia matamshi ya Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ambaye ameashiria kushindwa mradi wa kusambaratisha Muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia na kusema kwamba, licha ya takriban mashambulizi ya anga 10,000 katika vita vya “Al-Asf al-Maakul” nchini Lebanon, Muqawama umeendelea kubakia imara na madhubuti.

Sheikh Naim Qassem, amesema, Marekani lazima isitishe mradi wa Israel, na akaongeza kusema kuwa, “Nina hakika kwamba Israel itaporomoka na kusambaratika kutokea ndani, na kile inachofanya sasa ni dhulma kubwa dhidi ya ubinadamu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *