
Maambukizi 1,003 ya Ebola yamerekodiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo mlipuko wa hivi karibuni umesababisha pia vifo vya watu wasiopungua 254.
Hii ni takwimu mpya iliyotolewa jana na taasisi ya Taifa ya Afya ya Umma ya DRC (INSP) kufuatia mlipuko wa Ebola uliotangazwa Mei 15 mwaka huu.
Karibu visa vyote vya maambukizi vimeripotiwa katika jimbo la Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini maeneo yanayokumbwa na migogoro ya makundi yenye silaha.
Virusi hivyo pia vimeenea hadi nchi jirani ya Uganda, ambapo Shirika la Afya Duniani WHO limerekodi visa 20 na vifo viwili, ingawa serikali mjini Kampala ilisema mapema mwezi huu kuwa ugonjwa umedhibitiwa. Mlipuko huu wa Ebola unatokana na aina adimu ya virusi vya Bundibugyo ambayo haina chanjo au matibabu rasmi.
Idadi ya visa halisi inaaminika kuwa kubwa zaidi kwa sababu mlipuko huo ulithibitishwa kwa kuchelewa kwa wiki kadhaa.
Jitihada za kukabiliana na virusi hivyo zimekabiliwa na changamoto kutokana na ukosefu wa chanjo au matibabu yaliyoidhinishwa ya spishi ya Bundibugyo ya virusi hiyo inavyosababisha mlipuko wa sasa.
Majanga ya kiafya ya hivi karibuni, likiwemo janga la COVID-19, yamepelekea kuzidishwa juhudi za kuongeza uzalishaji wa chanjo barani Afrika, lakini bado hakuna mafanikio makubwa yaliyopatikana.