KIUNGO mkabaji wa Azam FC, Himid Mao baada ya kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja, ames-ema matarajio yake msimu ujao ni kuongeza juhudi zaidi ili kuhakikisha kiwango chake kinaendelea kuwa bora.
Mao aliyefunga bao moja katika ushindi wao 3-2 dhidi ya Yanga katika nusu fainali ya Kombe la CRDB, alisema kiwango alichokionyesha msimu huu kimeonekana na sasa anachokizingatia zaidi ni nidhamu, bidii na kujituma ili kuhakikisha ubora wake uwanjani hauporomoki.
“Ligi ya msimu huu ina changamoto kubwa ya ushindani. Kocha anapokuamini na kukupa nafasi ya ku-cheza lazima ujue kuna mwingine benchi anayesubiri, hivyo ni muhimu kujituma na kulinda kiwango chako,” alisema Mao.
Aliongeza, wachezaji wa Azam FC bado wana imani ya kupambania kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara katika mechi zilizosalia.
“Mbali na hilo, wachezaji wa Azam bado tuna imani ya kumaliza nafasi ya pili katika ligi. Tunajua ni ngu-mu, lakini inawezekana endapo tutafanya vizuri katika mechi zilizosalia,” alisema.
Azam FC imebakiza mechi tatu muhimu dhidi ya Yanga Juni 24, Coastal Union Juni 27 na Dodoma Jiji Juni 30. Mao anaamini endapo watazishinda mechi zote hizo na Simba ikapoteza pointi sita, wanaweza ku-maliza nafasi ya pili.
Alisema lengo jingine kubwa ni kuhakikisha timu inapata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, hatua ambayo anaamini itawapa uzoefu zaidi na kuimarisha uwezo wa kikosi hicho katika mashindano ya kimataifa.
Kwa sasa, Simba SC ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 64, huku Azam FC ikiwa nafasi ya tatu kwa alama 58.
Mao ni miongoni mwa wachezaji wenye historia ndefu katika klabu hiyo. Kwa mara ya kwanza aliichezea Azam FC kati ya mwaka 2008 hadi 2018, kabla ya kujiunga na Petrojet (2018/19), ENPPI (2019-2021), Ghazl El Mahalla (2021-22) na Talaea El Gaish SC (2022-2025).
Baadaye alirejea Azam FC na kusaini mkataba wa mwaka mmoja na baada ya kuonyesha kiwango kizuri akapatiwa mkataba mwingine utakaomfanya abaki hadi msimu wa 2026/27.
Katika historia yake na Azam FC, Mao amewahi kuwa sehemu ya mafanikio ya klabu hiyo, ikiwemo kushinda Kombe la Kagame mwaka 2018 baada ya kuifunga Simba SC mabao 2-1.
Pia alisaidia timu kutwaa mataji ya Kombe la Mapinduzi katika nyakati tofauti, na alikuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wakati Azam FC ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2014.