California, Marekani. Timu ya taifa ya Algeria, imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Jordan katika mechi kali na ya kuvutia ya kundi J kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026, ikiwa ni ushindi wa kwanza wa kikosi hicho baada ya kupita miaka 12.
Kabla ya ushindi huo, mara ya mwisho kwa Algeria kushinda mechi ya Kombe la Dunia ilikuwa ni hatua ya makundi dhidi ya Korea Kusini ilipoichapa mabao 4-2, Juni 22, 2014, katika fainali za michuano hiyo zilizofanyika Brazil.
Katika mechi hiyo ya kundi J, iliyopigwa kwenye Uwanja wa San Francisco Bay Area Kaskazini mwa California, Jordan ilianza kupata bao dakika ya 36, lililofungwa na kiungo wa timu hiyo, Nizar Al-Rashdan aliyemalizia pasi ya Mousa Al-Tamari.
Licha ya Algeria kutengeneza nafasi nyingi na kumiliki zaidi mpira, lakini Jordan ilicheza kwa nidhamu ya hali ya juu iliyochangia kuipeleka timu hiyo hadi dakika 45 za kwanza ikiongoza bao 1-0, ikiwa ni historia kwa kikosi hicho katika michuano ya Kombe la Dunia.
Baadhi ya wachezaji wa Algeria wakishangilia ushindi katika Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Jordan. Picha na Mtandao
Kipindi cha pili Jordan iliendelea kucheza kwa nidhamu ya kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza ingawa ilishindwa kumudu presha ya Algeria na kuruhusu bao la kusawazisha dakika ya 69, lililofungwa na Nadhir Benbouali aliyemalizia pasi ya Riyad Mahrez, kisha Amine Gouiri akafunga la pili dakika ya 82 na kuihakikishia timu hiyo ushindi wa kwanza baada ya siku 4,384.
Jordan ilianza michuao hiyo kwa kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Austria kama ilivyokuwa pia kwa Algeria iliyochapwa 3-0 dhidi ya Argentina huku ikishuhudiwa Lionel Messi akifunga ‘Hat-Trick’ ya kwanza ya Kombe la Dunia 2026.
Kabla ya leo, mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa ni mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyopigwa Mei 30, 2004 na kuisha sare ya bao 1-1, ambapo bao la Algeria lilifungwa na Abdelmalek Cherrad huku la Jordan likifungwa na Mahmoud Shelbaieh.
Matokeo hayo yanaifanya Algeria kufikisha pointi tatu katika msimamo wa kundi J sawa na Austria nyuma ya vinara Argentina yenye pointi sita, huku Jordan ikiwa mkiani bila pointi.
Algeria maarufu kwa jina la ‘Les Fennecs’, imekuwa moja ya timu kutoka Afrika muhimu katika historia ya Kombe la Dunia, ambapo kikosi hicho kinashiriki michuano hiyo mara ya tano tangu mwaka 1982, 1986, 2010, 2014 na 2026.
Katika ushiriki wake wa kwanza wa Kombe la Dunia lililofanyika Hispania mwaka 1982, Algeria iliishangaza dunia baada ya kuifunga Ujerumani Magharibi iliyoongoza kundi la pili kwa mabao 2-1, ingawa iliishia makundi kwa kumaliza nafasi ya tatu.
Timu hiyo ilirejea tena Kombe la Dunia mwaka 1986, lililofanyika Mexico na kuangukia kundi D, lililokuwa na timu za Brazil iliyoongoza, Hispania na Ireland ya Kaskazini, ambapo kikosi hicho kiliburuza mkia baada ya kupata pointi moja.
Baadhi ya wachezaji wa Algeria wakishangilia ushindi katika Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Jordan. Picha na Mtandao
Baada ya kushiriki fainali hizo za 1986, Algeria iliichukua miaka 24, kushiriki Kombe la Dunia lililofanyika Afrika Kusini mwaka 2010 na kumaliza pia mkiani mwa kundi C, nyuma ya vinara, Marekani, England na Slovenia.
Mafanikio bora kwa Algeria ni kufika hatua ya 16 bora katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, lililofanyika Brazil na kuchapwa na Ujerumani mabao 2-1, baada ya dakika ya 120, kutokana na ndani ya dakika 90 matokeo kuwa 0-0, Juni 30, 2014.
Kwa upande wa Jordan ilijaribu kwa miaka 40, kushiriki Kombe la Dunia bila ya mafanikio japo ilikaribia kufuzu mwaka 2014 na kushindwa katika hatua ya mtoano, baada ya kikosi hicho kuchapwa na Uruguay mabao 5-0, katika mechi iliyopigwa Novemba 13, 2013.
Hata hivyo, Juni 5, 2025, ndio ilikuwa siku ya kihistoria kwa kikosi hicho baada ya kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, baada ya kuifunga Oman mabao 3-0, huku Ali Olwan akifunga mabao yote kwa maana ya Hat-Trick.