
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi wamekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Sayyid Badr bin Hamad al-Busaidi, kujadili utaratibu mpya wa kusimamia Lango-Bahari la kimkakati la Hormuz.
Qalibaf, ambaye aliwasili Muscat Jumatatu jioni baada ya mazungumzo ya Uswisi na ujumbe wa Marekani, anaongoza ujumbe wa Iran kwa mashauriano ya pamoja na maafisa wa Oman kuhusu usimamizi wa lango bahari hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman, pande hizo mbili zimejadili ushirikiano wa pande mbili na uhusiano mzuri wa ujirani mwema, na kuchunguza njia za kukuza uhusiano kwa maslahi ya pande zote mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ametangaza kwamba katika mkutano wake na Qalibaf na Araghchi, pande mbili zimefanya majadiliano yenye kujenga kuhusu vifungu vya mkataba wa maelewano uliosainiwa na Tehran na Washington, hasa masuala yanayohusiana na Lango-Bahari la Hormuz.
“Msisitizo wetu ulikuwa katika kutetea sheria za kimataifa na kuhakikisha meli zinapita salama,” amesema Badr al-Busaidi.
Pande zote mbili zimesisitiza umuhimu wa kutumia fursa ya sasa ya kidiplomasia kuunga mkono juhudi za amani na kuimarisha utulivu na amani, kwa kuzingatia kanuni na sheria za kimataifa na ujirani mwema.
Iran na Oman zimesisitiza kwamba ushirikiano huo utazidisha fursa za kupunguza misukosuko na kulinda usalama wa kikanda, pamoja na usalama wa baharini katika Lango-Bahari la Hormuz na njia za maji za kimataifa.
Ziara hiyo inakuja huku kukiwa na mvutano mkubwa wa kikanda kuhusu usalama wa baharini katika Lango-Bahari la Hormuz, eneo muhimu la usafirishaji wa mafuta duniani, huku Iran ikitaka kuwekwa utaratibu mpya wa usimamizi baina yake na jirani yake wa Ghuba ya Uajemi.