Dar es Salaam. Kauli ya mwanamuziki wa Bongo Fleva, Rayvanny, kwamba aliwahi kufanya kazi na staa wa Marekani Jason Derulo kabla ya Diamond Platnumz, imezua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii. Baadhi ya mashabiki wakihoji madai hayo, na kusema msanii huyo anajipa sifa asizostahili.
Hata hivyo, kumbukumbu za miradi ya muziki zinaonyesha kuwa Rayvanny alikuwa miongoni mwa wasanii wa Afrika waliopata nafasi ya kushirikiana na Jason Derulo kupitia mradi wa Coke Studio Africa mwaka 2017/2018.
Kupitia mradi huo, walishiriki kurekodi na kutumbuiza wimbo wa “Push Up On It”, pamoja na wasanii wengine wa Afrika akiwemo Bebe Cool kutoka Uganda na Dela kutoka Kenya.
Ushirikiano huo ulimpa Rayvanny fursa ya kufanya kazi moja kwa moja na nyota huyo wa Marekani katika mazingira ya ubunifu wa muziki.
Mahusiano yao ya kikazi yaliendelea hata baada ya Coke Studio, ambapo mwaka 2018 Rayvanny alishirikiana na Jason Derulo kwenye remix ya wimbo “Tip Toe”.
Ushirikiano huo unaelezwa kuwa ulitokana na ukaribu na uelewano walioujenga walipokutana kupitia jukwaa la Coke Studio Africa.
Kwa upande wa Diamond Platnumz, ushirikiano wake na Jason Derulo ulikuja baadaye kupitia mradi wa Coca-Cola katika wimbo ‘Colors’, uliotumika kuhamasisha Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2018.
Katika kampeni hiyo, Jason Derulo alirekodi matoleo tofauti ya wimbo huo akiwa na wasanii kutoka nchi mbalimbali, akiwemo Diamond Platnumz.
Kutokana na kumbukumbu hizo, madai ya Rayvanny yanaonekana kuwa na hoja. Kwani kupitia Coke Studio inaonyesha kuwa alikuwa tayari amefanya kazi na Jason Derulo kabla ya ushirikiano uliokuja baadaye kati ya msanii huyo wa Marekani na Diamond Platnumz.