Wachumi nchini Pakistan wamedai kuwa kipato cha mtu mmoja mmoja nchini humo kimeshuka hadi kufikia Rupia 8,484 kwa mwezi ambazo ni sawa na Shilingi 80,000 ya Tanzania.

‘’Asilimia 28.9 ya wananchi wanaishi chini ya mstari wa umaskini, kiwango cha juu zaidi katika muongo mmoja. Utafiti mdogo tulioufanya unaonesha takribani Wapakistan milioni 70 wako chini ya mstari huo,’’

‘’Hata ukifuatilia takwimu za Benki ya Dunia (WB) zinaonesha zaidi ya watu milioni 100 wanaishi chini ya Dola 4.20 kwa siku,’’ alisema Usman Hassan alipokuwa akitoa tathmini ya uchumi waliyoifanya kwa takribani miezi mitatu.

Wachumi hao wamekosoa mbinu ya kisiasa ya serikali kupunguza idadi ya masikini, wakisisitiza kuwa jambo muhimu linalopaswa kuzingatiwa ni kupunguza mfumuko wa bei, kuongeza mauzo ya nje na kuimarisha uwekezaji wa ndani.

Wakati hayo yakielezwa, hivi karibuni Waziri wa Fedha wa Pakistan, Muhammad Aurangzeb alikiri uwepo wa changamoto ya gharama za maisha inayowakabili wananchi, kuhusisha hali hiyo na mikakati ya kiuchumi inayoamuriwa na IMF.

‘’Tumekuwa tukikosoa mwenendo wa uchumi wa Pakistan lakini tunaona bado bajeti katika masuala ya ulinzi inaongezeka maradufu. Mivutano ya kikanda na shinikizo la IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa) vimetajwa kama sababu za uamuzi huo,’’ alisema Hassan.

Alidai uwiano wa kipato nchini humo ni mkubwa katika kipindi cha miaka 27, huku wastani wa mapato halisi ya kaya ukishuka kwa asilimia 12.

‘’Mwisho wa siku michezo hii ya takwimu haimlishi mtu yeyote, kwani umaskini halisi unazidi kuongezeka licha ya kubadilishwa kwa takwimu,’’ alisema akibainisha kuwa hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *