Burkina Faso imevunja uhusiano wa kidiplomasia na Ufaransa, na hivyo kuwa taifa jipya zaidi la Afrika Magharibi kujitenga na aliyekuwa mtawala wake wa kikoloni baada ya miaka ya kuzorota kwa mahusiano kati ya pande hizo mbili.

Uamuzi huo umetangazwa katika taarifa iliyotolewa Ijumaa na Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso, Gilbert Ouedraogo, na kuchapishwa kupitia huduma rasmi ya habari ya nchi hiyo. Taarifa hiyo imesema kuwa hatua hiyo ilianza kutekelezwa rasmi tarehe 26 Juni.

Burkina Fas inaishutumu Ufaransa kwa kufuatilia malengo ya ukoloni mamboleo, kuingilia mambo ya ndani, na kuunga mkono “mitandao ya hujuma” pamoja na “magaidi.”

Taarifa hiyo iimesema: “Tukiwa tumekabiliwa na malengo haya ya kiimla na ya kutaka kututawala, pamoja na kuwatia watu wetu katika utumwa, tumechagua uwajibikaji na mamlaka ya taifa letu.” Hapo awali, Ufaransa imekuwa ikikanusha tuhuma kwamba inaunga mkono ugaidi katika eneo la Sahel.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa uamuzi huo unahusu uhusiano wa kidiplomasia pekee, na hauathiri mahusiano ya kihistoria, kiutamaduni na kijamii kati ya wananchi wa Burkina Faso na wale wa Ufaransa.

Kwa mujibu wa AFP, Ufaransa imelaani hatua hiyo na kuieleza kuwa ni “uamuzi wa uhasama usio na msingi” unaoonyesha kile ilichokiita “mwelekeo wa kutia wasiwasi wa mamlaka ya Burkina Faso.”

Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Burkina Faso na Ufaransa yamekuwa yakizorota kwa kasi tangu jeshi lilipochukua madaraka mjini Ouagadougou mwaka 2022. Viongozi wapya walikatisha ushirikiano wa kijeshi na Paris, hatua iliyosababisha wanajeshi wa Ufaransa kuondoka nchini humo mwaka uliofuata.

Ufaransa imeendelea kupoteza ushawishi wake katika baadhi ya makoloni yake ya zamani, huku hisia za kupinga Ufaransa zikiongezeka kutokana na kile kinachoonekana ni sera za ubabe, uporaji madini na ukoloni mambo leo wa watawala wa Paris.

Burkina Faso, Mali, na Niger zimewafukuza wanajeshi wa Ufaransa na kuishutumu dola hiyo ya zamani ya kikoloni kwa kuunga mkono makundi yenye silaha yanayochochea uasi wa wanamgambo wenye itikadi kali ambao wamesababisha maafa makubwa katika ukanda huo.

Ufaransa imekanusha mara kadhaa tuhuma hizo, na kusema haitambui uhalali wa tawala za kijeshi katika nchi hizo tatu za Afrika Magharibi, huku ikiunga mkono juhudi za kurejesha utawala wa kiraia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *