
Singida. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Singida, imewahukumu wanaume wawili wakazi wa Kata ya Iganson wilaya ya Ikungi mkoani Singida, akiwemo kaka mtu aliyekodi wauaji kwa Sh1.8 milioni ili kumuua dada yake.
Mwanamume huyo alikodi wauaji na kuwalipa malipo ya awali ya Sh800,00 kwa kile alichodai dada yake ‘amemfunga’ kishirikina kiasi kwamba uume wake ulianza kuwa mdogo na uliendelea kupungua na kuingia ndani.
Hukumu hiyo ya kifo dhidi ya Wilson Masingija au Gunda na Samwel Mwaka au Mwema, ilitolewa Juni 25, 2026 na Jaji Nenelwa Mwihambi na kuwekwa katika tovuti ya Tanzlii Juni 26, 2026.
Moja kati ya ushahidi uliowatia hatiani kwa kosa la kuua kwa kukusudia, ni maelezo ya ungamo ya washitakiwa waliyoyatoa polisi, walieleza hatua kwa hatua mipango ilivyosukwa, wauaji walivyolipwa na mauaji yalivyotekelezwa.
Kwa mujibu wa ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri, mauaji hayo yalitokea Agosti 4, 2024 katika Kijiji cha Unyange, Kata ya Iglanson wilaya ya Ikungi mkoani Singida, ambapo walishtakiwa walimuua Rebeca Masingja kwa kumkata kwa panga.
Siku ya tukio saa 2:00 usiku, shahidi wa kwanza, Christina Magaka alikuwa jikoni akipasha chakula kwa ajili ya mama mkwe wake, Rebeca Masingija au Gunda (marehemu) alikuwa nje ya nyumba yao na ndugu zake wengine wawili.
Wakati huo wanafamilia wengine walikuwa ndani sebuleni, lakini ghafla watu wawili wakiwa wameshika mapanga walitokea na kuanza kumkata kwa panga Rebeca, ambapo shahidi huyo na wanafamilia wengine walikimbia kujiokoa.
Walikimbilia katika nyumba ya jirani yao aitwaye Fuku, na baadaye walijulishwa kuwa Rebeca alifariki pale pale katika eneo la tukio.
Agosti 5, 2024, polisi wakiwa wameambatana na shahidi namba 2, Dk Musa Munya walifika eneo la tukio na katika uchunguzi ilibainika sababu za kifo ni majeraha kichwani na mkononi, yaliyosababishwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali.
Shahidi namba 3, G.8587 Koplo Sixtus aliyekuwa mmoja wa wapelelezi, alisema yeye ndiye aliyemkamata mshitakiwa wa kwanza (Wilson), baada ya kupokea kwa taarifa fiche kuwa alihusika katika mauaji hayo.
Kwa upande mwingine, shahidi namba 4, Inspekta Luck Mwakyelu, yeye alieleza namna alivyomkamata mshitakiwa wa pili (Samwel Mwaka), Desemba 18,2024, akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Iglansoni.
Shahidi namba 5, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dominic Mayala ndiye aliyeandika maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa kwanza wakati Staff Sajini Frank aliandika maelezo ya mshitakiwa wa pili, na wote walikiri kosa.
Maelezo yao yalipokelewa mahakamani kama kielelezo P2 na P3.
Maelezo ya ungamo
Mshitakiwa wa kwanza alinukuliwa akieleza kuwa “Februari 2, 2024 tulionana na dada yangu tangu tulipopigana na alinitamkia kwamba hutokaa uzae tena na huyo mtoto ulienaye ndiyo wa mwisho, hutokuwa mwanaume tena na huzai”.
“Baada ya siku chache toka amenitamkia maneno hayo nilianza kuona dalili ambazo uume wangu ulianza kuwa mdogo kwa kusinyaa na kuingia ndani kadri siku zinavyokwenda uume wangu ukawa unaingia ndani yaani tofauti na mwanzo na hali hiyo nimeendelea kuwa nayo hadi sasa,”aliendelea kueleza:-
Katika maelezo hayo aliendelea kusimulia “Baada ya kuona hivyo nilianza kutafuta msaada wa kupona tatizo langu kwa kuuliza watu mbalimbali kama wanafahamu dawa ya kurudisha uume wangu, lakini sikuweza kufanikiwa hadi sasa.
“Baada ya kushindwa kupata dawa ya kutibu tatizo langu nikatafuta watu kwa ajili ya kumuua dada yangu Rebeca Masingija Gunda ambaye ndiye chanzo cha tatizo langu na pia amekuwa kikwazo katika maisha yangu,” alisimulia.
Alidai kuwa Julai 21, 2024 alikutana na mtu aitwaye Kulwa na mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Samweli Mwaka au Mwama, baada ya kuwaeleza shida yake, walikubaliana malipo ya kazi hiyo ni Sh1.8 milioni.
Julai 29, 2024 alikutana tena na watu hao na kuwalipa malipo ya awali ya Sh800, 000 na kuwapa ramani nzima na mwonekano wa dada yake na kuwaelekeza nyumba anayoishi ambapo walikwenda kutekeleza mauaji hayo.
Mshitakiwa wa pili katika maelezo yake, anasimulia tukio hilo kwa maudhui yanayofanana na ya Wilson na kueleza namna mtu aitwaye Kulwa alivyomtafuta na kumweleza kuwa kuna mtu anataka wamsaidie kumuua dada yake.
“Nakumbuka tarehe 04.08.2024 ilikuwa siku ya mpira kati ya Yanga na Simba. Tuliondoka mimi na Kulwa kuelekea nyumbani kwa dada yake na Wilson, ili kufanya kazi aliyotutuma. Mimi nilikuwa na panga, Kulwa alikuwa na tochi.”
“Tuliegesha pikipiki karibu na nyumba yake na tulishuka kwenye pikipiki kisha tulisogea kwa miguu karibu na nyumba ya dada yake na Wilson. Ilikuwa yapata 2:00 usiku. Tulijibanza nje ya nyumba. Tuliwaona watu watatu wanakula.
“Tulipokaribia, mwenzangu aliwasha tochi na nilimuona mlengwa alikuwa amekaa, alipoona mwanga wa tochi alijaribu kuamka lakini kabla hajaamka nilimsogelea karibu na kumkata kwa panga kichwani mara mbili na alianguka chini, baada ya kuanguka chini wale wenzake wakakimbia wakipiga mayowe.
“…Nakumbuka tarehe 07.08.2024 alikuja Kulwa nyumbani na kunieleza kwamba Wilson amekamatwa na Polisi, hivyo hela iliyobakia baada ya kazi sijui tutaipataje? Tulikubaliana kila mtu akae kwa tahadhari … Ukweli mimi nimekuwa natumiwa au kukodiwa kufanya mauaji wilaya ya Iramba na Manyoni,” mwisho wa kunukuu.
Hata hivyo katika utetezi wake, mshitakiwa wa kwanza alikana kushiriki kufanya mauaji hayo lakini akakiri kuna wakati kulikuwa na kutokuelewana na ndugu yake, lakini kuliisha na akakana kuandika maelezo polisi ambako alikiri kutenda kosa.
Badala yake alidai aliteswa na aliposhindwa kuvumilia mateso alikubali kusaini maelezo na kuieleza mahakama kuwa hamfahamu kabisa mshitakiwa wa kwanza na kwamba alikutana naye kwa mara ya kwanza mahakamani Machi 3, 2025.
Kama ilivyokuwa kwa mshtakiwa wa kwanza, mshitakiwa wa pili naye alikanusha kutenda kosa hilo na kwamba alikamatwa kuhusiana na mauaji ya mtu mwingine kabisa aitwaye Shaban Mreni na mkewe, yanayodaiwa kutokea Aprili 4, 2024.
Mshitakiwa huyo alieleza kuwa wakati anahojiwa kuhusiana na mauaji hayo, aliteswa na maofisa wa polisi iliakiri mauaji hayo, kwamba hakuhojiwa kuhusiana na mauaji ya Rebeca na hamfahamu mshitakiwa wa kwanza.
Hukumu ya mahakama
Katika hukumu yake, Jaji Mwihambi alisema hakuna ubishi kuwa Rebeca ni marehemu na kifo chake si cha kawaida na kwamba majeraha mabaya aliyoyapata yanathibitisha kuwa kifo chake kilikuwa cha mateso na kibaya.
Jaji alisema swali muhimu ni kama washitakiwa ndio waliosababisha kifo chake na kama ni kwa dhamira ovu ambapo mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa pasipo kuacha mashaka, kuwa wao ndio waliomuua marehemu kwa nia ovu.
Jaji alisema ingawa hakuna mtu aliyeshuhudia washitakiwa wakifanya mauaji hayo, ushahidi ukiunganishwa kwa ujumla wake, yakiwamo maelezo yao ya kukiri kosa, yanawatia hatiani washitakiwa na kosa hilo.
“Maelezo ya kukiri ya washtakiwa (kielelezo P2 na P3) yanafunua uhasama wa muda mrefu wa mshtakiwa wa kwanza dhidi ya marehemu, pamoja na mpango na utekelezaji halisi wa tukio hilo. Zikichukuliwa pamoja, mambo haya yanathibitisha wazi kwamba mshtakiwa wa kwanza na wa pili walitenda kosa hilo kwa nia ovu,”alisema.
Jaji Mwihambi aliukataa utetezi wa washitakiwa na kuwatia hatiani kwa mauaji ya kukusudia ambapo alieleza kuwa kwa sheria za Tanzania, adhabu kwa mtu anayepatikana na kosa la mauaji ni moja tu, nayo ni kunyongwa hadi kufa.