MASHABIKI wa Simba ni kama wanaonekana hawajafurahishwa na hatua ya mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kupelekwa Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba wakipiga kelele mitandaoni juu ya ugumu wa kufika huko, lakini uongozi wa klabu hiyo umetoa tamko.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Juni 25 mwaka huu lilitangaza Uwanja wa Gombani kuwa ndio utakaotumika kwenye fainali ya michuano hiyo ambapo Simba itacheza dhidi ya Azam kuanzia saa 11:00 jioni.
Simba iliing’oa Coastal Union kwa jumla ya mabao 4-0 kwenye mchezo wa nusu fainali iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, huku Azam ikimuondoa bingwa mtetezi Yanga kwa mabao 3-2 kwenye nusu fainali iliyopigwa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori amesema wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa mashabiki wao juu ya uamuzi wa uwanja wa fainali hiyo.
Magori amesema Simba haipingi uamuzi wa TFF, lakini wanaona mashabiki wao wengi hawajatendewa haki akiamini watakumbana na ugumu wa kufika Pemba kutokana na gharama kubwa.
“Ni kweli tumeona mashabiki wengi wakilalamika, tumewaambia hatuna nafasi ya kubadili hilo kwa kuwa wenye mamlaka ya kuamua mchezo huo unachezwa wapi ni Shirikisho, tunatakiwa kuheshimu hilo,” amesema.
“Ukitazama malalamiko yao utaona yana msingi, soka linapendezeshwa na mashabiki wanavyojaa viwanjani, ukifikiria gharama za kufika Pemba utaona kwamba ni kweli kutakuwa na kazi kubwa watu wengi kufika huko.
“Uongozi tunasimamia kuipeleka timu lakini huku nako tunakutana na ugumu namna ya kuweka mazingira tulivu ya watu wote kukaa pamoja, tumeanza kuwatawanya baadhi.
“Mashabiki pia watapata shida hiyo ya kupata sehemu zenye unafuu kwenye malazi kwa kuwa haiwezi kuwa safari ya siku moja kufika Pemba na kurudi kwenye familia zao.
“Nadhani wakati mwingine wenzetu wanatakiwa kuliangalia hili, tunaona kwamba utaweza kuwapa nafasi mashabiki wachache, unaweza kuangalia kama Unguja tu Kuna ugumu, je vipi Pemba.”
Aidha Magori amewatuliza mashabiki wa Simba akiwataka kupambana kwenda kuipa nguvu timu hiyo ikitafuta taji lingine msimu huu kwenye fainali hiyo itakayopigwa Julai 4, 2026.
Hii itakuwa fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la CRDB kuikutanisha Simba na Azam, huku timu zote zikiwa na shauku ya kubeba ubingwa huo ambao kwa misimu minne mfululizo ulichukuliwa na Yanga.
Tangu msimu wa 2015-2016 ambapo mashindano hayo yalirejea kwa jina la Azam Sports Federation Cup baada ya kusimama kwa takribani miaka 12 kuanzia 2003 hadi 2015, tayari Azam imecheza fainali nne, ikishinda moja msimu wa 2018-2019 ilipoichapa Lipuli bao 1-0.