Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaambia viongozi wapya aliowaapisha watambue wamebeba dhamana hivyo wanapaswa kuwa waadilifu na kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi na si kwenda ofisini kupumzika.

Rais Samia ameyasema hayo baada ya kuwaapisha viongozi hao wateule leo Jumatano, Julai Mosi, 2026, Ikulu Dar es Salaam katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu.

Walioapishwa ni Dk Grace Magembe, ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya. Kabla ya uteuzi huo, Dk Magembe alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali.

Charles Kadonya, aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

Pia, Nolasco Kipanda aliyeapishwa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma ambaye kabla ya uteuzi huo, alikuwa akihudumu kama Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Taasisi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

“Mna bahati kwakuwa mmeapa leo na mnaanza kazi leo siku ambayo tunaanza utekelezaji wa dira yetu ya maendeleo ya miaka 25 ijayo kwa hiyo mjue kwamba mnaingia si kwenda kupumzika bali ni mchakamchaka sababu dira hii lazima tuitekeleze kwa kasi,” amesema.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Grace Elias Magembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Julai 1, 2026.    .

Alichomwambia Dk Magembe

Kutokana na uzoefu wake katika utumishi nafasi mbalimbali sekta ya afya, Rais Samia amemwambia Dk Magembe akafanye kazi aliyompa ya ukatibu mkuu.

“Umekuwa hatua kwa hatua katika wizara hii, unaijua vizuri mafanikio na changamoto zake na umekutana na wenzio unawajua vizuri, imani yangu utatoa ushirikiano mkubwa. Ninyi madaktari mna mambo yenu mnajuana madaktari wakikukataa hautaweza kufanya kazi sasa na wewe ni daktari nenda kafanye na madaktari wenzio,” amemwambia.

“Unakwenda kuanza kazi ikiwa ndio kwanza tumepitisha bajeti na kama unavyojua bajeti siku zote huwa haitoshi kulingana na vipaumbele vya wizara kwa hiyo uvijue vizuri vipaumbele vya wizara changamoto nenda katumie bajeti hii kwa uangalifu lakini tupate matokeo makubwa na kwa spidi,” amesisitiza.

Amesema nchi imeamua kuwa na utoshelevu wa dawa na vifaatiba angalau kwa asilimia 60 hadi itakapofika mwaka 2030 na kuna watu wanakuja kwa hiyo wakaribisheni wawekezaji waweke viwanda anayetaka vifaatiba anayetaka madawa lakini kwa ubora hivyo itasaidia kulinda fedha.

Rais Samia amemwambia Kadonya, “Nenda mkafanye kazi kwa pamoja mhakikishe Jumuiya inakwenda vizuri na masilahi ya Tanzania ndani ya jumuiya mkayalinde vyema.”

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimuapisha Nolasco Jacob Kipanda kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Julai 1, 2026.   

Kipanda atwishwa zigo migogoro watumishi wa umma

Kwa upande wake, Kipanda aliyeapishwa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma ameambiwa akawe mwadilifu kusimamia haki kwa kutoa uamuzi sahihi.

“Huku kuna kazi kidogo kuna mashauri ya watumishi kuna malalamiko na migogoro, kinachotakiwa ni uadilifu kusimamia katika misingi ya haki, hakikisha tume yako inatoa uamuzi kwa misingi ya haki anayefanya makosa ahukumiwe kwa makosa yake ambaye hajafanya tume isimame katikati,” amesisitiza.

Amesema migogoro iliyopo huko ni kutokana na uamuzi, mtumishi anaweza kuhukumiwa kwa chuki, hivyo akasimamie haki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *