
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu bwabwaja za Rais Donald Trump dhidi ya wananchi wa Iran kwa kusisitiza kuwa, shughulikia utapiamlo wa watu milioni 40 nchini Marekani, na usihamishie matatizo yako kwa wengine.
Mohammad Bagher Qalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amechapisha andiko katika mtandao wa kijamii ujumbe kwa lugha ya Kiingereza akisema: ‘shughulikia tatizo la zaidi ya wananchi milioni arobaini wa nchi yako ambao wanategemea mgao wa chakula (mpango wa msaada wa chakula wa serikali), lakini wakati huohuo unaita nchi nyingine kuwa “nchi yenye njaa.”
Spika Qalibf aliongeza: Kauli hii si tangazo au madai ya kawaida; hii ni kuepuka kuwajibika. Yaani mnahamisha matatizo yenu kwa wengine.
Qalibaf alisisitiza: Nasaha na maelekezo yenu kuhusu mpango wa SNAP (mpango wa msaada wa chakula wa Marekani) bakieni nayo wenyewe.
Aliendelea kusema: Sisi wenyewe tunaamua kuhusu rasilimali na mali zetu; nyinyi fikirieni kuhusu kiwango cha utapiamlo katika nchi yenu wenyewe.”
Katika miaka ya hivi karibuni, mjadala kuhusu hali ya maisha nchini Marekani umeongezeka, hasa kuhusu suala la ukosefu wa uhakika wa chakula (food insecurity). Ingawa Marekani ni moja ya nchi tajiri zaidi duniani, takwimu zinaonyesha kuwa mamilioni ya watu bado wanakumbwa na changamoto ya kupata chakula cha kutosha na cha mara kwa mara.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, kati ya asilimia 10 hadi 13 ya kaya nchini humo hukumbwa na changamoto ya kupata chakula cha kutosha kwa vipindi tofauti vya mwaka, hali inayowakilisha zaidi ya watu milioni 30 hadi 40 katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi duniani.
Ripoti zinaeleza kuwa ongezeko hilo limechangiwa zaidi na kupanda kwa gharama za maisha, ikiwemo bei ya chakula, kodi za nyumba, pamoja na mfumuko wa bei ulioshuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni. Aidha, ajira zisizo na uhakika na mishahara isiyokua kwa kasi sawa na gharama za maisha zimeelezwa kuwa sababu nyingine zinazochangia hali hiyo.