Kahama. Serikali wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, imeendesha operesheni maalumu ya kubomoa ukuta uliokuwa umejengwa katika eneo la shule ya awali na msingi, uliodaiwa kuziba njia ya wananchi na kuzunguka makazi ya watu bila ridhaa yao.
Operesheni hiyo imekuja kutokana na mvutano ulioanza siku chache zilizopita kati ya mamlaka za Serikali ya Mtaa wa Kitwana na mmiliki wa shule hiyo, baada ya kudaiwa kujenga ukuta na kuingilia hifadhi ya barabara, licha ya kuwepo kwa mazungumzo ya awali yaliyohusisha viongozi wa serikali ya mtaa na kata.
Akizungumza wakati wa tukio hilo jana jioni, Julai 5, 2026, mjumbe wa Mtaa wa Kitwana, Michael Mayila, amesema suala hilo lilishindikana kutatuliwa kupitia mazungumzo ya awali, hali iliyosababisha serikali ya mtaa kuchukua hatua za utekelezaji katika ngazi ya wilaya.
Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kahama ikiendelea na ukaguzi wa mipaka ya eneo linalomilikiwa na mwekezaji wa shule ya binafsi, Steven Nyeriga, katika Mtaa wa Kitwana, Kata ya Busoka, muda mfupi kabla ya kubomolewa kwa ukuta uliokuwa umejengwa na kuziba barabara ya wananchi, baada ya mmiliki kushindwa kuubomoa kwa hiari. Picha na Amina Mbwambo.
“Sisi kama serikali ya mtaa, hili limekuwa changamoto. Tumejaribu kuzungumza naye, lakini ukaidi ukaendelea. Kama wananchi wataachwa hivi, tutasumbuka zaidi. Ndiyo maana tumeshukuru Serikali ya wilaya kuingilia kati na kuhakikisha linatatuliwa.”
Kwa upande wake, mkazi wa mtaa huo, ambaye nyumba yake ilizungushiwa ukuta, Joyce Paskali, amesema wamekuwa wakinyanyaswa na jirani yao ambaye ni mmiliki wa shule hiyo, kutokana na eneo hilo kudhibitiwa kwa namna iliyozua hofu na migogoro.
Shughuli ya ubomoaji wa ukuta uliokuwa umejengwa kuziba barabara ya wananchi ikiendelea katika Mtaa wa Kitwana, Kata ya Busoka, Wilaya ya Kahama, baada ya Kamati ya Usalama ya Wilaya kusimamia utekelezaji wa hatua hiyo kufuatia mmiliki kushindwa kuubomoa kwa hiari.
“Tunashukuru sana Serikali kwa kutusaidia. Tulikuwa tunanyanyaswa. Ukitaka kujenga, anakulazimisha uhame, akupe pesa au hata asikupe, lakini uhame.”
Mkazi mwingine, Abduli Mugendi, ameeleza kuridhishwa na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya wilaya, akisema imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanyonge waliokuwa hawana sauti mbele ya mwekezaji huyo.
Ameiomba Serikali kuendelea kusimamia matumizi sahihi ya ardhi ili kuhakikisha migogoro ya aina hiyo haijirudii tena.
“Tumeteseka sana kama wananchi. Tunashukuru Serikali kwa kutuona na kutusaidia, maana hii ni hatua nzuri kwa wananchi ambao hatuna nguvu, ni wanyonge.”
Msingi wa nyumba wa Emanuel Godfrey uliozungushiwa ukuta na mmiliki wa shule ya kibinafsi Steven Nyeriga katika mtaa wa Kitwana kata ya Busoka Manispaa ya Kahama, wakati akiendelea na ujenzi.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kazi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amesema Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote atakayekaidi maagizo halali ya mamlaka za umma, akisisitiza kuwa sheria lazima ifuatwe.
“Serikali ipo kwa ajili ya wananchi wote. Pale ambapo maagizo yanatolewa na yakakaidiwa, hatutakuwa na namna nyingine zaidi ya kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake ili kulinda maslahi ya umma na kuhakikisha amani inaendelea,” amesema Nkinda.
Nkinda ametoa onyo kwa wawekezaji na watu wenye uwezo wa kifedha kufanya shughuli zao kwa kuheshimu na kutii sheria za nchi, hususan katika masuala ya ardhi, ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika.
Ukuta huo ni ule uliojengwa kuziba barabara ya wananchi na kuzunguka makazi ya watu bila ridhaa yao na mwekezaji wa shule binafsi katika Mtaa wa Kitwana, Kata ya Busoka, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Shughuli ya ubomoaji wa ukuta uliokuwa umejengwa kuziba barabara ya wananchi ikiendelea katika Mtaa wa Kitwana, Kata ya Busoka, Wilaya ya Kahama, baada ya Kamati ya Usalama ya Wilaya kusimamia utekelezaji wa hatua hiyo kufuatia mmiliki kushindwa kuubomoa kwa hiari.
Mmiliki wa eneo hilo, Steven Nyeriga, aliiomba kamati impatie muda ili azungumze na majirani zake kuhusu kuwapa fidia, suala ambalo viongozi wa mtaa pamoja na wananchi walilipinga vikali.
“Mkuu wa wilaya, msinibomolee. Mimi hawa wananchi wenye maeneo nitamalizana nao, tunafahamiana. Mmeshabomoa upande ule, nimekubali; huku niacheni. Kama ni gharama za hati mpya, nitatoa, lakini si kunibomolea mbele ya usimamizi wote huu,” amesema.
Hata hivyo, ombi hilo halikukubaliwa na wananchi hao.