
Admeri Habibullah Sayyari Naibu Mratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa jaribio lolote la majeshi ya kigeni kutua katika pwani ya Iran litakabiliwa na jibu kali sana, na kuonya kuwa ukanda wa pwani ya Iran utageuka kuwa “jehanamu” kwa jeshi lolote vamizi.
Akizungumza leo katika mahojiano yaliyorushwa katika televisheni ya taifa, Admeri Sayyari ameeleza kuwa jaribio lolote la kutua wanajeshi wa nchi ajinabi katika ardhi ya Iran ni mstari mwekundu kwa taifa la Iran, na kwamba Marekani ilikuwa imepanga operesheni kama hiyo lakini ikashindwa kuitekeleza.
Amesema, jeshi la Iran pamoja na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Polisi, Basiji na wananchi wa Iran vimejiandaa kikamilifu kuilinda nchi na kwamba hakuna hoja yoyote inavyoweza kuipatia ujasiri Washington wa kufanya oparesheni kama hiyo.
Kamanda Habibullah Sayyari ameongeza kuwa: Adui anafahamu kwamba akifanya upumbavu wa namna hiyo kwa wanajeshi wake kutua katika pwani ya Iran atatumbukia katika jehanamu ambayo hakuna njia ya kutokea.
Wakati huo huo Admeri Sayyari ametupilia mbali madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba jeshi la Wanamaji la Iran limeangamizwa na kusema:
Amesema, matamshi ya Washington yalikusudia kuonyesha kuwa ukanda wa pwani ya Iran uko hatarini kuingiliwa kijeshi.
Amesema, Marekani inapigana vita vya kisaikolojia kupitia taarifa za kukaririwa zenye lengo la kuwatisha wananchi wa Iran.
Naibu Mratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewahakikishia wananchi wa Iran vikosi vya ulinzi vya nchi hii vinaendelea kujitayarisha kikamilifu kuilinda nchi na kwamba mipaka ya Iran iko salama na hakuna tishio dhidi ya mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya Iran litakalovumiliwa.