
Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imeonya kwamba saratani inaweka mzigo mkubwa wa kibinadamu na kiuchumi kwa jamii duniani kote, ikichukua uhai wa zaidi ya watu 26,000 kila siku na kudhihirisha ukosefu mkubwa wa usawa katika viwango vya maisha kati ya nchi tajiri na maskini.
Wataalamu wanasema fursa ya kuokoka saratani mara nyingi hutegemea mahali mtu anapoishi. Ingawa mtu mmoja kati ya wanne barani Ulaya na Amerika Kaskazini anatarajiwa kupata saratani, ni karibu mtu mmoja kati ya 12 pekee ndiye anayeaga dunia kutokana na ugonjwa huo. Hata hivyo, barani Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara, matokeo ni mabaya zaidi kwa sababu ya huduma ndogo za utambuzi na matibabu ya mapema ya sratani.
Ripoti hiyo inaangazia tofauti kubwa iliyopo katika takwimu za watu wanaonusurika saratani ya matiti. Katika nchi zenye kipato cha juu, karibu asilimia 90 ya wanawake wanaogunduliwa na ugonjwa huo huishi kwa angalau miaka mitano. Katika nchi zenye kipato cha chini, takwimu hiyo inashuka hadi zaidi ya asilimia 40.
Manusura wa saratani ya matiti na mtetezi wa waathirika wa ugonjwa huo Abigail Simon-Hart amesema upatikanaji wa bima ya matibabu ya kibinafsi ulimuwezesha kupata matibabu ya haraka nchini Uingereza, lakini ameonya kwamba wagonjwa wengi katika nchi kama vile Nigeria wanakabiliana na uchunguzi wa kuchelewa, huduma duni za afya na matatizo makubwa ya kifedha.
Kutokana na kuwepo takriban visa vipya milioni 20.6 vya saratani na vifo karibu milioni 10 kila mwaka vinavyosababishwa na maradhi hayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema utambuzi wa kila mwaka wa wagonjwa wa saratani unaweza kuongezeka hadi karibu milioni 35 ifikapo mwaka 2050 kama hatua za haraka hazitachukuliwa ili kupanua huduma za kinga, kuboresha matibabu na kupunguza ukosefu wa usawa duniani katika kutoa huduma ya saratani.