Cape Town. Rais na Mtendaji Mkuu wa MeTL Group, Mohammed Dewji ameelezea namna alivyofanya mageuzi ya biashara ya familia yao kwa kipindi cha karibu miongo mitatu, hadi sasa kuwa miongoni mwa kampuni kubwa barani Afrika yenye mapato ya karibu Sh8trilioni.

Dewji anasema METL ambayo ilianzishwa zaidi ya nusu karne iliyopita, ilianza kwa msingi wa biashara ndogo, ambapo babu na bibi zake walikuwa wafanyabiashara wa rejareja wakiuza chumvi na bidhaa nyingine za matumizi ya kila siku katika duka dogo lililokuwa kijijini nchini Tanzania.

Baadaye baba yake alipanua shughuli hizo kwa kuanzisha biashara ya usafirishaji wa bidhaa katika kipindi ambacho miundombinu ya nchi ilikuwa bado haijaendelea, hatua iliyoweka msingi wa ukuaji wa kampuni hiyo.

Kutoka kwenye duka hilo dogo la rejareja, baba yake alifanikiwa kuwa na biashara yenye Dola milioni 30 (Sh70.9 bilioni) kwa mwaka, Mo anasema hatua hiyo ilihitaji uthabiti, azma isioyumba na imani kubwa na imani hiyohiyo ndiyo inayoendelea kumpa msukumo hadi leo.

Akizungumza katika mkutano wa biashara ulioandaliwa na Benki ya Standard Group (Africa Unlocked 2026) uliofanyika jijini Cape Town, alisema mwaka 1998 alipochukua nafasi ya kuendeleza biashara hiyo, aliona kuwa biashara ya uchuuzi pekee isingeweza kuijengea Afrika uchumi imara.

“Niliporejea Tanzania baada ya kuhitimu Georgetown University, wengi walitarajia niendelee kupanua biashara yetu ya usambazaji. Badala yake, tuliamua kuwekeza katika viwanda vya ndani wakati ambao wengi hawakuona huo kama uamuzi sahihi,” alisema.

Alieleza kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa MeTL pia imechangiwa na kununua viwanda vilivyokuwa vikisuasua wakati Tanzania ilipotekeleza sera ya ubinafsishaji, kama sehemu ya mageuzi ya uchumi wa soko na kampuni yao ilifanikiwa kuvigeuza kuwa biashara zenye faida.

“Badala ya kukaa ofisini kwenye mazingira ya starehe, nilitumia muda mwingi viwandani nikifanya kazi pamoja na wafanyakazi wetu, ili kufufua biashara zilizokuwa zikidorora na kuzigeuza kuwa shughuli za uzalishaji zenye mafanikio. Tuliona fursa mahali ambapo wengine waliona matatizo, tukawekeza katika teknolojia mpya, mifumo bora na watu ili kuvifanya viwanda hivyo kuwa na tija,” alisema.

Ingawa MeTL ilianza kama kampuni ya biashara iliyokuwa ikichuuza bidhaa muhimu nchini Tanzania, Dewji alisema waligundua kuwa ustawi wa kudumu usingeweza kupatikana kwa kutegemea biashara hiyo pekee ambayo inahusisha kuagiza na kusambaza bidhaa za nje.

Kutokana na mkakati huo, MeTL Group ilipanua shughuli zake katika usindikaji wa vyakula, uzalishaji wa mafuta ya kula, vinywaji, nguo, sabuni, dawa za kufulia na bidhaa nyingine za matumizi ya kila siku zinazotumiwa na mamilioni ya Waafrika.

Mbali na viwanda, alisema kampuni hiyo pia imewekeza katika sekta za usafirishaji, benki na bima ili kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa shughuli zake na kuwa bidhaa zao za vinywaji baridi zimeleta ushindani mkubwa sokoni kiasi cha kuzipiku chapa kubwa kama Pepsi na Cocacola.

Dewji alisema siri nyingine ya mafanikio ya kampuni hiyo imekuwa ikibadilika kulingana na mazingira ya biashara, huku ikikabiliana na mabadiliko ya bei za bidhaa duniani, kuyumba kwa thamani ya fedha, mabadiliko ya sera na kanuni pamoja na mahitaji ya walaji.

“Masoko hubadilika, uchumi hubadilika na mahitaji ya wateja hubadilika. Lakini kanuni yetu imebaki ileile, kujenga biashara zinazotatua matatizo ya watu. Ukifanya hivyo, soko litafuata,” alisema bosi huyo wa METL ambayo sasa inazalisha bidhaa zaidi ya 51 katika mataifa 11 barani Africa.

Alisisitiza kuwa ukuaji wa biashara hauwezi kupatikana bila ushirikiano, akieleza kuwa mafanikio ya MeTL Group yametokana na imani waliyopewa na Watanzania, Waafrika pamoja na washirika wa biashara kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo India na China.

“Hakuna mjasiriamali anayefanikiwa peke yake. Hakuna kampuni inayokua peke yake. Hakuna taifa linaloendelea peke yake. MeTL Group imekuwa ilivyo leo kwa sababu ya watu na washirika walioona uwezo wetu, hususan Watanzania na Waafrika waliotuunga mkono katika safari yetu,” alisema Mo.

Hata hivyo, alisema ingawa upatikanaji wa mitaji ni muhimu kwa biashara lakini mafanikio ya wajasiriamali hutegemea zaidi uthubutu, kujiamini na ustahimilivu.

 “Mtaji ni muhimu. Lakini kujiamini na ustahimilivu ni muhimu Zaidi,” alisema.

Urejeshaji kwa umma

Kwa mujibu wa Dewji, mafanikio ya biashara yanapaswa kwenda sambamba na uwekezaji kwa jamii, ndiyo maana kupitia Mo Dewji Foundation amewekeza katika elimu, afya na upatikanaji wa maji safi.

Alisema taasisi hiyo imetoa zaidi ya ufadhili 450 wa masomo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kutibu zaidi ya wagonjwa 120,000, kufanya zaidi ya upasuaji wa macho 10,000 pamoja na kusaidia watoto wanaoishi na saratani na wale wanaozaliwa na matatizo mbalimbali.

“Baada ya miaka mingi ya uzoefu, nimegundua kuwa kujenga kunahusu mambo mengi zaidi ya kufanya biashara. Biashara huzalisha ustawi wa kiuchumi. Uhisani hupanua fursa. Michezo hujenga imani na matumaini,” alisema Mo.

Alisema kupitia MeTL Group, Taasisi ya Mo Dewji Foundation na uwekezaji wangu katika Klabu ya Simba, lengo halijawahi kuwa kujenga taasisi zenye mafanikio pekee. Lengo limekuwa kujenga taasisi zinazowaendeleza watu, kufungua uwezo wao, kukuza vipaji na kuwaandaa vijana wa kizazi kijacho ili wafikie mafanikio makubwa zaidi kuliko tuliyoyafikia sisi.

“Mwisho wa siku, urithi wetu mkubwa hautakuwa biashara tulizozijenga, bali utakuwa watu ambao biashara hizo zimewasaidia kuwajenga. Sekta zinaweza kubadilika, lakini dhamira hubaki ileile. Kujenga si tukio la mara moja, bali ni mtazamo wa maisha. Ni uamuzi wa kuacha mahali, jamii au taasisi ikiwa bora zaidi kuliko ulivyoikuta,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *