Askari usalama katika eneo lililojitenga na Somalia la Somaliland wamemkamata mwanamuziki kijana, Khalid Mohamud Abdillahi, anayejulikana sana kama Khalid Kamil, baada ya kutunga wimbo kuhusu al-Quds iliyokaliwa kwa mabavu. Hayo yameripotiwa na Hiiraan Online, ikinukuu familia yake.

Kaka yake, Abdimajid Mohamud Abdillahi, amesema Kamil ameshikiliwa bila kesi kwa wiki mbili zilizopita.

Abdimajid amesema maafisa wa ujasusi walimkamata mwanamuziki huyo nyumbani kwake Hargeisa kabla ya kumhamishia Idara ya Upelelezi wa Jinai. Amesema, baadaye Kamil alihamishiwa Gereza Kuu.

“Walimkamata Khalid nyumbani kwake,” Abdimajid amesema na kuongeza: “Idara ya Ujasusi ilimshutumu kuimba wimbo kuhusu Quds inayokaliwa kwa mabavu ambao bado hajautoa.”

Abdimajid amesisitiza kuwa: “Askari usalama walituambia kwamba Khalid anashikiliwa kwa kutunga wimbo, lakini kwa kuwa wimbo huo hauhusu Somaliland, bali unahusu Quds, tunaona kwamba kuna mtu anayechochea au anayehusika na kukamatwa kwake”.

Chama cha upinzani cha Somaliland cha KAAH kimelaani kukamatwa huko, kikikutaja kuwa ni ukiukwaji wa uhuru wa msingi na sehemu ya kampeni pana ya kukandamiza ukosoaji wa sera ya serikali kuhusu “Israel”.

“Kukamatwa wasanii, waandishi wa habari na raia kwa kutoa maoni na ubunifu wao kunadhoofisha uhuru wa msingi unaodhaminiwa na katiba,” chama hicho kimesema.

Hapo awali mamlaka ya Somaliland iliwakamata viongozi wa kidini, wazee wa kitamaduni, waandishi wa habari na wanaharakati vijana ambao walipinga hatua ya utawala katili wa Israel ya kutambua rasmi Somaliland kama nchi inayojitawala. Baadhi ya waliokamatwa baadaye waliachiliwa huru bila kufunguliwa mashtaka.

Kaka yake Kamil anasema, mashairi ya wimbo huo yanajumuisha mistari inayosema kwamba al-Quds “imeporwa” na inawakosoa wale wanaokaa kimya kuhusu uhalifu huo.

Kukamatwa msanii huyo kunakuja baada ya Somaliland kufungua ofisi ya kidiplomasia huko al-Quds inayokaliwa kwa mabavu na Israel mwezi uliopita wa Juni, miezi sita baada ya “Israel” kuripotiwa kuitambua Somaliland kama “taifa huru”.

Israel ilitangaza kuitambua rasmi Somaliland kama dola huru mnamo Desemba 2025, hatua ambayo Somalia iliipinga na kuilaani vikali, ikiitaja kuwa ni “shambulio la makusudi dhidi ya mamlaka na uhuru wa Somalia.”

Aidha nchi za Afrika, Kiarabu na Kiislamu duniani zimepinga vikali hatua ya utawala wa Israel kuanzisha uhusiano na eneo la Somaliland ambalo ni sehemu ya Somalia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *