MOROGORO: WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amemuagiza mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Bigwa–Kisaki (km 78) kuhakikisha anafanya matengenezo ya mara kwa mara katika maeneo yanayotumiwa na wananchi wakati ujenzi ukiendelea, ili kuondoa adha ya usafiri na kupunguza gharama za usafirishaji.

Ulega alitoa agizo hilo, juzi mkoani Morogoro, alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.

Pia alitoa maelekezo ya kwa TANROADS na mkandarasi kuhakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote, hata ujenzi ukiwa unaendelea.

Alisema haikubaliki kwa wananchi kuendelea kutumia barabara yenye mashimo makubwa wakati mkandarasi yupo eneo la mradi, akisisitiza kuwa matengenezo ya mara kwa mara ni sehemu ya wajibu wake.

“Ni lazima barabara ipitike vizuri katika eneo lote ambalo ujenzi unaendelea. Hili si jambo la hiari, bali ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha wananchi hawapati usumbufu,” alisema Ulega.

Alisema kuwa hakuna sababu ya kuiacha barabara ikiwa na mashimo mengi kiasi cha kushindwa kupitika, akisisitiza kuwa matengenezo ya kawaida lazima yafanyike wakati wote ili wananchi waendelee kupata huduma bora za usafiri.

Waziri Ulega alimuelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro kuhakikisha anamrejesha mkandarasi katika barabara ya Kinole–Madamu (km 10) haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kufanya matengenezo ya dharura na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Shaban Taletale, ameueleza Waziri kuwa wananchi wana imani na Serikali katika kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ili waweze kupata huduma bora za usafiri na kufikiwa na maendeleo yaliyokusudiwa.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Patrick Rambika, alisema ujenzi wa barabara ya Bigwa–Kisaki ulianza mwezi Septemba 2025 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2027.

Mhandisi Rambika alisema kuwa mradi huo unatekelezwa na mkandarasi China Railway 15 Bureau Group Corporation chini ya usimamizi wa TECU.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *