
Jeshi la Sudan limesema mapema Jumanne kuwa limekomboa eneo la Fashfoun katika jimbo la Blue Nile baada ya mapigano na waasi wa makundi ya RSF na SPLM-N.
Katika taarifa, jeshi hilo lilisema kuwa vikosi vya Brigedi ya 13 chini ya Divisheni ya 4 ya Askari wa Miguu, vikisaidiwa na vikosi vya Operesheni Maalumu, “vimesafisha” eneo la Fashfoun baada ya “mapambano ya makali yaliyoisababishia hasara kubwa kwa waasi.”
Jeshi limeongeza kuwa vikosi vyake vinaendelea na operesheni za msako na ulinzi kwa lengo la kuwafuatilia wapiganaji wa RSF waliosalia na kurejesha usalama na uthabiti katika eneo hilo.
Tangazo hilo limekuja siku chache baada ya jeshi kusema kuwa lilikuwa limekomboa mji wa kimkakati wa mpakani wa Al-Kurmuk tarehe 8 Julai.
Jeshi la Sudan linadhibiti maeneo makubwa ya jimbo la Blue Nile, huku waasi wa SPLM-N ambao wamekuwa wakipambana na serikali tangu mwaka 2011, wakitaka utawala wa kujitawala kwa maeneo ya South Kordofan na Blue Nile.
Makundi ya waasi wa RSF na SPLM-N yameunda muungano wa pamoja katika jimbo la Blue Nile Sudan dhidi ya Jeshi la Sudan (SAF).
Sudan imekumbwa na mzozo tangu Aprili 2023, wakati mapigano yalipozuka kati ya jeshi na RSF kuhusu mpango wa kukiunganisha kikosi hicho cha wanamgambo ndani ya jeshi la taifa. Vita hivyo vimesababisha mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani, vikiua makumi ya maelfu ya watu na kuwafanya mamilioni kuhama makazi yao. Serikali ya Sudan inasema waasi watenda jinai wa RSF wanapata uungaji mkono wa kifedha na silaha kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).