
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5
Kombe la Dunia sasa limefikia hatua za mwisho za mashindano.
Moja kati ya Ufaransa, Hispania, Argentina au England itatawazwa kuwa bingwa wa dunia Jumapili hii jijini New York.
Lakini ni nani atakayeshinda?
Je, mechi ya nusu fainali kati ya Ufaransa na Hispania siku ya Jumanne ndiyo fainali halisi, kama wengi wanavyodai? Je, Argentina inaweza kuwa timu ya tatu tu katika historia kutetea taji lake la dunia? Au England itamaliza miaka 60 ya kusubiri ubingwa?
BBC Sport imezungumza na waandishi wa habari pamoja na mashabiki kutoka nchi zinazoshiriki ili kujua wanadhani nini kitatokea.
“Huenda huu ukawa mwaka wa England” – mtazamo kutoka Hispania
Guillem Balague, mwandishi wa habari kutoka Hispania:
Hispania – ndiyo timu bora zaidi.
Ufaransa – wana mchezaji bora zaidi na safu ya ushambuliaji inayotisha zaidi.
Argentina – wana mfumo bora zaidi wa kucheza, wakifanya mengi kwa kutumia rasilimali chache kuliko timu nyingine yoyote.
England – wana wachezaji wawili wa kiwango cha dunia ambao wako katika kiwango bora kwa sasa.
Timu zote nne zilizofika hatua ya nusu fainali zina kila kinachohitajika ili kutwaa ubingwa.
Iwapo Hispania itaweza kuinyang’anya Ufaransa mpira na kuzuia mashambulizi yao ya kushtukiza, pamoja na kuwa makini zaidi kutumia nafasi wanazopata, wana nafasi kubwa ya kufuzu fainali.
Hata hivyo, italazimika kucheza mchezo mkamilifu, huku Lamine Yamal akiwa katika kiwango cha juu kabisa.
Argentina itajaribu kufanya mechi dhidi ya England isiwe na matukio mengi, kisha kusubiri wakati wa ubora wa Lionel Messi au Julián Álvarez kuamua matokeo. Lakini wamekuwa wakicheza kwa kujiweka katika hatari.
England bado inatafuta utambulisho wake wa uchezaji, lakini ina moyo mkubwa wa kupambana na nyota wawili wa kiwango cha dunia.
Fainali kati ya Hispania na England itakuwa ya kusisimua sana. Kwa upande wangu, nitafurahia matokeo yoyote, lakini ningependa England ishinde Kombe la Dunia hivi karibuni. Huenda huu ukawa ndiyo mwaka wao.
Mashabiki wa Hispania nchini Marekani:
Lionel: “Ufaransa watakuwa wapinzani wagumu, lakini naamini tunaweza kuwashinda. Tukifanya hivyo, tutakuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa. Tuna safu imara ya ushambuliaji na ulinzi. Kitu pekee kinachotia wasiwasi ni kwamba Pedri bado hajacheza katika kiwango hiki cha juu.”
Jack: “Argentina wanaonekana kuwa imara, lakini England hawawezi kupuuzwa. Wana Harry Kane, ambaye ni mmoja wa washambuliaji hatari zaidi duniani.”
Michel: “Hispania watashinda mashindano haya, sina shaka hata kidogo. Watu wengi hawatupi nafasi dhidi ya Ufaransa, lakini tutadhibiti mchezo na kuwashinda. Mshindi wa mechi hiyo ndiye atakayekuwa bingwa wa mashindano.”
“Ni vigumu kuiona timu nyingine ikiipita Ufaransa” – mtazamo kutoka England
Ningependa sana kusema England, lakini kutokana na ushahidi wa kile tulichokiona hadi sasa kwenye Kombe hili la Dunia, naamini Ufaransa watafuta machungu ya kupoteza dhidi ya Argentina nchini Qatar mwaka 2022 kwa kutwaa ubingwa safari hii.
Kwa maoni yangu, England itafuzu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966 kwa kuifunga Argentina.
Hata hivyo, ni vigumu sana kuipuuza Ufaransa kutokana na ubora wao mkubwa wa kushambulia. Kylian Mbappe anaonekana kuwa na dhamira ya kutwaa taji, huku akisaidiwa na wachezaji kama Ousmane Dembele, Michael Olise na Desire Doue.
Na bado kuna Bradley Barcola na Rayan Cherki, ambao walikuwa benchi wakati Ufaransa ilipoiondoa Morocco katika robo fainali.
Kwa hiyo, ninaona fainali ikiwa kati ya England na Ufaransa, ambapo Didier Deschamps ataaga kwa kutwaa Kombe la Dunia. Lakini utabiri wangu umewahi kuwa si sahihi hapo awali, hivyo bado kuna matumaini makubwa kwa kocha wa England, Thomas Tuchel, na wachezaji wake.
Mashabiki wa England nchini Marekani;
Paul: “Kombe linarejea nyumbani. Kwa kweli! Kwa nini isiwe hivyo? Tunajua England haijacheza vizuri sana, lakini tuna Jude Bellingham na Harry Kane, na naamini hiyo itatosha. Sioni Argentina wakituzuia, halafu fainali dhidi ya Ufaransa au Hispania itakuwa na nafasi sawa kwa pande zote.”
Dean: “Ningependa kuwa na imani hiyo, lakini ninaona ugumu. Tulionekana kusumbuliwa na majeraha na uchovu katika mechi dhidi ya Norway, na hilo linaanza kutuathiri. Naona Lionel Messi anaweza kuharibu ndoto yetu.”
Kane: “Ufaransa watashinda Kombe la Dunia. Sisi wengine ni washindani wa kawaida tu. Je, England wataifunga Argentina? Inawezekana, lakini kwa shida. Hata hivyo, hawataweza kuifunga Ufaransa.”
“Kuna imani kubwa” – mtazamo kutoka Ufaransa
Abdoul-Karim, mwandishi wa habari wa TV5 Monde kutoka Ufaransa:
Hatujui kabisa cha kutarajia kutoka kwa Hispania, hasa kwa Lamine Yamal, ambaye ameonekana kutokufikia kiwango kilichotarajiwa mwanzoni mwa mashindano. Hata hivyo, ana uwezo wa kuamka na kung’ara dhidi ya Ufaransa.
Lakini nchini Ufaransa kuna imani kubwa. Safari hii hakuna mabishano wala migogoro inayozunguka timu. Mambo yamekwenda kwa utulivu zaidi ikilinganishwa na mashindano makubwa yaliyopita.
Karibu nchi nzima ya Ufaransa itasimama kutazama nusu fainali hii. Jumanne ni Siku ya Bastille, na katika baadhi ya miji maonesho ya fataki yameahirishwa ili yafanyike baada ya mechi. Wafaransa wengi wanatumaini kuwa watakuwa wakisherehekea kufuzu kwa timu yao kwenda fainali nyingine ya Kombe la Dunia.
Mashabiki wa Ufaransa nchini Marekani:
Rachel: “Hii ndiyo timu bora zaidi ya Ufaransa ambayo nimewahi kuiona. Tunapaswa kushinda Kombe la Dunia kwa sababu sisi ndio bora, ingawa tunajua hakuna ushindi wa uhakika. Hispania ni wapinzani hatari, na natarajia kukutana na England kwenye fainali.”
Gerard: “Bila shaka tutashinda Kombe la Dunia. Hamjatuona tukicheza? Sisi ni bora zaidi kuliko timu nyingine zote.”
“Ufaransa wako hatua moja mbele ya kila timu nyingine” – mtazamo kutoka Argentina
Santi Sciola, mwandishi wa habari kutoka Argentina:
Nadhani Ufaransa ndiyo timu yenye nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa. Katika safu ya ushambuliaji wana kikosi kinachotia hofu kwa kila mpinzani, na kadiri mashindano yanavyoendelea wameendelea pia kuimarika katika safu ya ulinzi.
Bila shaka ninatamani Argentina ishinde ubingwa. Wanaweza kufanya hivyo kwa urahisi kwa sababu ni timu inayocheza kwa moyo mkubwa. Lakini kwa ubora wa soka kwa sasa, naiona Ufaransa ikiwa hatua moja mbele ya timu nyingine zote.
Mashabiki wa Argentina nchini Marekani:
Emma: “Tuna imani. Haitakuwa rahisi, lakini England pia wanajua haitakuwa rahisi kwao. Sikumbuki mara ya mwisho walipokutana kwa sababu bado nilikuwa mdogo. Lakini ninajua England hawajawahi kukabiliana na Messi katika kiwango hiki, naye ndiye mchezaji wetu wa kipekee. Nafikiri tutashinda kwa mikwaju ya penalti, lakini tutapoteza dhidi ya Ufaransa kwenye fainali.”
Javier: “Bila shaka tutashinda. Tumepitia mechi ngumu lakini tumefanikiwa kuvuka. Tunaweza kuifunga England na, tukifika fainali, hatutapoteza.”
Bruno: “Haiwezekani kutabiri. England wana wachezaji bora sana, huku Hispania na Ufaransa wakionekana kuwa timu zenye nguvu zaidi. Lakini mimi nasema Argentina ndiyo watakaoshinda ubingwa.”