Dar es Salaam. Wakati mahitaji ya wataalamu wa teknolojia, mabadiliko ya tabianchi na uchumi wa buluu yakizidi kuongezeka nchini na duniani, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeanzisha programu mpya 29 kwa mwaka wa masomo 2026/2027, hatua inayolenga kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Kuanzishwa kwa programu hizo kunakuja wakati Tanzania ikiendelea kuweka msisitizo katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kisasa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na mipango ya kuimarisha uchumi unaotegemea maarifa na ubunifu.

Programu hizo ni sehemu ya programu 120 zitakazotolewa katika mwaka mpya wa masomo baada ya kufanyika mapitio ya mitaala ili kuendana na uhitaji wa soko la ajira kwa sasa duniani.

Miongoni mwa kozi mpya zitakazotolewa ni Shahada ya Sayansi ya Uchambuzi wa Takwimu na Akili Unde, Shahada ya Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi na Usimamizi wa Maliasili, Shahada ya Sayansi ya Afya ya Mazingira na Uendelevu pamoja na Shahada ya Sayansi ya Bahari (Oceanography).

Katika eneo la uchumi wa buluu, chuo hicho pia kitaanza kutoa Stashahada ya Ikolojia ya Utalii wa Pwani na Bahari pamoja na Stashahada ya Teknolojia ya Ufugaji wa Viumbe Baharini, hatua inayotarajiwa kuongeza wataalamu katika sekta hiyo inayokua kwa kasi.

Mbali na kozi za sayansi na teknolojia, UDSM pia imeanzisha programu zinazolenga kukuza taaluma za sayansi za jamii na ubunifu, ikiwemo Shahada ya Siasa na Utawala wa Umma, Shahada ya Uchumi, Shahada ya Tafsiri na Ukalimani pamoja na Shahada ya Fasihi na Uandishi wa Ubunifu.

Programu nyingine mpya ni Shahada ya Sayansi ya Kemia, Shahada ya Sayansi ya Bioteknolojia ya Chakula na Shahada ya Historia, Nyaraka na Urithi, ambazo zote zitatolewa katika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce) kilichopo Iringa.

Akizungumzia hilo, Mratibu wa Kurugenzi ya Shahada za Awali, Dk Geradius Kikumi amesema hatua hiyo ni mwelekeo wa chuo kuendana na mahitaji mapya ya maendeleo ya taifa, hususan katika nyanja za uchumi wa kidijitali, ulinzi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi, afya ya mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

Wanafunzi wakijisomea katika eneo linalojulikana lama Mdegree katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Mbali na programu hizo mpya, tumefanya maboresho ya mitaala ya programu zote 120 za shahada ya kwanza ili ziendane na mahitaji ya sasa ya soko la ajira na maendeleo ya teknolojia,” amesema Dk Kikumi.

Mratibu huyo ameeleza kuwa chuo pia kitaendesha dirisha maalumu la kutoa huduma za ushauri na msaada kwa waombaji kuanzia Julai 20 hadi Julai 25 katika maktaba mpya ya UDSM.

Wasemavyo wadau

Mtaalamu wa elimu, Dk Magdalena Shirima amesema maboresho hayo yanaonyesha vyuo vikuu vinaanza kujibu kwa vitendo changamoto ya pengo la ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

Amesema kwa muda mrefu waajiri wamekuwa wakilalamikia upungufu wa wataalamu wenye uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutatua changamoto zinazotokana na mabadiliko ya mazingira.

“Kuanzishwa kwa programu kama Akili Unde na Sayansi ya Takwimu ni hatua muhimu kwa sababu karibu kila sekta sasa inategemea matumizi ya data kufanya maamuzi. Wahitimu wa fani hizi watakuwa na nafasi kubwa katika sekta za fedha, afya, biashara, kilimo na utawala,” amesema.

Hata hivyo, amesema mafanikio ya programu hizo yatategemea uwekezaji katika miundombinu ya kufundishia, vifaa vya kisasa na walimu wenye uwezo wa kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

“Siyo tu kuongeza idadi ya kozi, bali ni kuhakikisha wanafunzi wanapata ujuzi wa vitendo unaowawezesha kushindana ndani na nje ya nchi,” amesema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa sera za elimu, Patric Msuya amesema kuanzishwa kwa kozi zinazohusu uchumi wa buluu na sayansi za bahari ni fursa kubwa kwa Tanzania kutokana na kuwa na rasilimali nyingi za bahari ambazo bado hazijatumika ipasavyo.

Amesema sekta ya uchumi wa buluu ina uwezo wa kuleta ajira kupitia uvuvi wa kisasa, utalii wa bahari, ufugaji wa viumbe baharini na tafiti za rasilimali za bahari.

“Tanzania ina eneo kubwa la bahari, lakini bado tuna upungufu wa wataalamu wenye ujuzi wa kutosha katika eneo hili. Kozi kama Oceanographyna Teknolojia ya Ufugaji wa Viumbe Baharini zinaweza kusaidia kujenga kizazi kitakachoweza kutumia rasilimali hizo kwa maendeleo ya taifa,” amesema Msuya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *