
Wapalestina 14 wameuawa na wengine 37 kujeruhiwa, wengi wao wakiwa katika kambi ya Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza, kutokana na mashambulizi mtawalia ya Israel yaliyolenga maeneo mbalimbali ya ukanda huo, huku hali ya kibinadamu ikizidi kuwa mbaya.
Mashambulizi hayo ni sehemu ya ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano unaoendelea kufanywa na Israel tangu Oktoba 10, 2025.
Vyanzo vya habari katika hospitali za Ukanda wa Gaza vimeripoti kuwa watu 14 wameuawa na wengine 37 kujeruhiwa katika mashambulizi tofauti ya askari wa Israel.
Hospitali ya Al-Awda imetangaza kuwa shambulio la anga la Israel limelenga msafara wa mazishi katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza, na kuwaua Wapalestina 8 na kujeruhi wengine 20.
Ripoti zinasema kwamba ndege zisizo na rubani za Israel zililenga mkusanyiko wa Wapalestina waliokuwa wakiomboleza shahidi katika Msikiti wa Ahmed Yassin katikati ya kambi ya Nuseirat kwa makombora zaidi ya moja, na kusababisha vifo vya Wapalestina 8 na majeraha ya wengine zaidi ya 20, wakiwemo wanawake, watoto na wazee, huku majeraha ya 10 kati yao yakitajwa kuwa mabaya.
Ripoti hizo zimesema kuwa ndege ya kijeshi ya Israel pia imelenga hema la wakimbizi katika mji wa Al-Zawaida, jambo lililosababisha kifo cha Mpalestina mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.
Kwa upande wake, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Israel katika kambi ya Nuseirat, katikati mwa Ukanda wa Gaza, baada ya kulipua kwa mabomu mkutano wa raia wakati wa mazishi ya mmoja wa mashahidi wa Kipalestina, na kusababisha vifo vya mashahidi wasiopungua 8.
Harakati hiyo imekariri wito wake kwa wapatanishi wa makubaliano ya kusitisha mapigano na Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka ili kukomesha “ugaidi wa Kizayuni, mashine ya mauaji na mzingiro wa utawala katili” dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa data za hivi karibuni za Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza, ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano wa Israel hadi Alkhamisi wiki hii, umesababisha vifo vya Wapalestina 1,127 na kujeruhi wengine 3,643.