
Mjumbe wa ngazi za juu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kwamba Saudi Arabia imeweka uwezo na suhula zake za kisiasa, kifedha na kijeshi katika huduma ya miradi ya Marekani eneo la Asia Magharibi na inafanya kazi ya kudhoofisha mataifa ambayo yana misimamo dhidi ya Israel.
Muhammad al-Farah, mjumbe wa Idara ya Siasa ya Ansarullah, amesema kwamba utawala wa Saudi Arabia unaendelea kuwa bega kwa bega na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesema kwamba Saudi Arabia imeweka uwezo na suhula zake za kisiasa, kifedha na kijeshi katika kuhudumia miradi ya Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia na inafanya kazi ya kudhoofisha mataifa ambayo yanapinga utawala katili wa Israel.
Akizungumzia mashambulizi ya kijeshi na mzingiro wa kisiasa dhidi ya watu wa Yemen, Al-Farah amesema kwamba Riyadh inajaribu kukwepa nafasi yake ya moja kwa moja katika uchokozi na hujuma zinazofanywa dhidi ya watu wa Yemen.
Mwanachama huyo wa Idara ya Siasa ya Ansarullah amesema kuwa vikosi vya Jeshi la Yemen viko macho, na hatua inayofuata itashuhudia maendeleo ya uwanjani ndani ya mfumo wa kukabiliana na uchokozi.
Huku akieleza imani yake ya kupata ushindi, afisa huyo wa harakati ya Ansarullah amesisitiza kwamba utawala wa Saudi Arabia “utakabiliwa na matokeo mabaya ya sera zake dhidi ya Yemen.”