‎#HABARI: Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limewahimiza wamiliki na madereva wa vyombo vya moto kutumia mfumo wa kidijitali wa MIMIS kufanya maombi ya ukaguzi wa kila mwaka na kupata stika ya usalama barabarani kwa njia ya mtandao.

‎Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Mtaalamu wa Mifumo wa Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu, Inspekta Elisha Ernest, amesema mfumo wa MIMIS unaratibu mchakato mzima wa ukaguzi wa vyombo vya moto pamoja na utoaji wa stika za usalama barabarani kwa njia ya kidijitali.

‎Amesema mwombaji anatakiwa kujisajili kwenye mfumo kwa kuingiza taarifa zake binafsi, ikiwemo majina, jinsia na namba ya simu, kisha kujaza taarifa za chombo cha moto, kuchagua aina ya ukaguzi, mkoa, wilaya na tarehe anayotarajia kufanyiwa ukaguzi.

‎Baada ya kuhakiki taarifa hizo, mfumo hutengeneza namba ya udhibiti (Control Number) kwa ajili ya malipo ya huduma. Gharama za ukaguzi ni shilingi 5,000 kwa gari binafsi, shilingi 7,000 kwa gari la biashara na shilingi 2,000 kwa pikipiki pamoja na bajaji. Malipo yanaweza kufanyika kupitia mitandao ya simu au kwa mawakala wa huduma za kifedha.

‎Baada ya malipo, mmiliki anatakiwa kupeleka chombo chake kwenye vituo vya ukaguzi vilivyotengwa na Jeshi la Polisi, ambapo wakaguzi watahakiki ubora wa chombo hicho. Kitakapokidhi viwango vya usalama kitapatiwa stika ya kidijitali, huku chombo kitakachobainika kuwa na kasoro kikielekezwa kufanyiwa marekebisho kabla ya kukaguliwa tena.

‎Matumizi ya mfumo huo yanalenga kurahisisha huduma za ukaguzi, kuongeza uwazi na ufanisi, pamoja na kuhakikisha vyombo vya moto vinavyotumika barabarani vinakidhi viwango vya usalama.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *