Dar es Salaam. Wadau wa afya wameiomba Serikali kuitambua rasmi taaluma ya Tiba ya Familia (Family Medicine) katika mfumo wa ajira za umma, wakisema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano katika hospitali za rufaa, kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya na kuboresha matibabu ya magonjwa sugu yanayoongezeka nchini.
Wito huo umetolewa wakati wa Mkutano wa Kumbukizi ya Benjamin William Mkapa uliofanyika Dar es Salaam kati ya Julai 14 na 16, 2026, ambapo Chuo Kikuu cha Aga Khan Tanzania (AKU) kilitumia jukwaa hilo kuhimiza kuimarishwa kwa huduma za afya ya msingi kupitia madaktari bingwa wa Tiba ya Familia.
Akizungumza na Mwananchi kando ya mkutano huo, Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa AKU, Maria Kisanko, amesema Tiba ya Familia ni suluhisho muhimu kwa changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya afya nchini.
Amesema tofauti na madaktari waliobobea katika taaluma moja, madaktari wa Tiba ya Familia hupata mafunzo yanayowajengea uwezo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo tiba ya ndani, afya ya watoto, uzazi na magonjwa ya wanawake, upasuaji na afya ya jamii.
Ofisa Utawala wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Evelyne Gasper (kulia), akifafanua jambo kwa wadau waliotembelea banda la chuo hicho katika kumbukizi ya Benjamin Mkapa iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam
Kutokana na ujuzi huo, Kisanko amesema wana uwezo wa kutambua, kutibu na kufuatilia magonjwa mbalimbali ya kawaida, pamoja na kubaini wagonjwa wanaohitaji kupewa rufaa kwa madaktari bingwa.
Hata hivyo, amesema hadi sasa taaluma hiyo bado haijatambuliwa rasmi katika mfumo wa ajira za Serikali, hali inayofanya wataalamu hao kunufaisha zaidi hospitali za binafsi ambazo tayari zinatambua mchango wao.
“Tunaendelea kushirikiana na watunga sera ili Tiba ya Familia iingizwe rasmi katika mfumo wa huduma za afya wa Serikali. Hii itasaidia kupunguza rufaa zisizo za lazima na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya,” amesema Kisanko.
Kwa mujibu wa Kisanko, umuhimu wa taaluma hiyo umeongezeka wakati Tanzania ikikabiliwa na ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kama kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na changamoto za afya ya akili, yanayohitaji ufuatiliaji wa muda mrefu badala ya wagonjwa kutegemea hospitali za rufaa pekee.
Amefafanua kuwa madaktari wa Tiba ya Familia hutoa huduma zinazomwangalia mgonjwa kwa ujumla, wakizingatia historia ya afya ya mtu binafsi pamoja na familia yake, hivyo kurahisisha uratibu wa huduma katika maisha yote ya mgonjwa.
Katika hatua nyingine, Kisanko amesema AKU inalenga kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kitabibu, uongozi, utafiti na ubunifu, huku ikiendelea kuwaunga mkono hata baada ya kuhitimu ili kuendeleza mawazo yatakayoboresha sekta ya afya.
Ofisa Utawala wa AKU, Evelyne Gasper, amesema kuimarishwa kwa Tiba ya Familia kutafanya huduma za afya kuanzia ngazi ya familia na jamii, jambo litakalosaidia kupunguza msongamano katika hospitali na kuimarisha kinga pamoja na udhibiti wa magonjwa.
Amesema madaktari wa Tiba ya Familia wana uwezo wa kushughulikia magonjwa mengi ya kawaida ya watoto, kufanya upasuaji mdogo na kutoa huduma ambazo kwa sasa husababisha wagonjwa wengi kufika hospitali za rufaa bila ulazima.
“Kutambuliwa kwa taaluma hiyo katika mfumo wa ajira za umma kutawanufaisha zaidi wananchi wa maeneo ya vijijini ambako bado kuna uhaba mkubwa wa madaktari bingwa,” amesema.
Amesema pamoja na kuimarisha Tiba ya Familia, ni muhimu pia kuendelea kuwekeza katika tafiti za afya na mafunzo ya ubobezi ili kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana haraka na milipuko ya magonjwa mapya na changamoto nyingine za kiafya.