IRINGA: Mkoa wa Iringa umeweka mkakati mpya wa kuharakisha mageuzi ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuelekeza nguvu katika uzalishaji unaozingatia mahitaji ya soko, matumizi ya teknolojia za kisasa na uongezaji thamani wa mazao, hatua inayolenga kuongeza kipato cha wananchi na kuifanya Iringa kuwa kitovu cha kilimo cha biashara nchini.

Mkakati huo umetangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, wakati akifunga rasmi Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) ya Mkoa wa Iringa yaliyodumu kwa siku nane, ambapo alisema mafanikio ya sekta hiyo hayawezi tena kupimwa kwa wingi wa mazao pekee, bali kwa uwezo wa kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi ushindani wa masoko ya ndani na kimataifa.

Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi, waoneshaji na wadau wa maendeleo, Kheri alisema Iringa imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba, rasilimali za maji na mazingira yanayowezesha uzalishaji mkubwa, hivyo kinachohitajika sasa ni kuunganisha nguvu za serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha ili kuongeza tija katika kila hatua ya uzalishaji.

“Ni lazima tubadili fikra kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha biashara. Tujifunze kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko, kutumia mbegu bora, kuongeza thamani ya mazao na kuwekeza katika usindikaji, uhifadhi na ufungashaji ili bidhaa zetu ziweze kushindana ndani na nje ya nchi,” alisema.

Alisema Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na wizara za kisekta, halmashauri, taasisi za utafiti na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za ugani zinaimarishwa, pembejeo zinapatikana kwa wakati na teknolojia zinafika kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na kipato.

Katika kuimarisha uchumi wa ndani, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wakurugenzi wa halmashauri na taasisi za umma kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa Iringa zinapewa kipaumbele katika ununuzi wa serikali, mradi zikidhi viwango vinavyotakiwa.

Alisema hatua hiyo itasaidia kukuza viwanda vidogo, kuongeza ajira na kuhakikisha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vinavyonufaika na mikopo ya halmashauri vinapata soko la uhakika.

Kheri pia alitangaza kuwa kuanzia maonesho ya mwaka 2027, Iringa itaanzisha mfumo wa ushindani utakaohusisha halmashauri, taasisi na waoneshaji binafsi ili kuongeza ubunifu, kuboresha ubora wa maonesho na kuyafanya yawe miongoni mwa maonesho bora nchini.

Mapema, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Elias Luvanda, alisema maonesho ya mwaka huu yameacha mafanikio makubwa kwa kuwajengea wakulima, wafugaji na wavuvi uelewa kuhusu masoko, kuongeza mitandao ya biashara na kuhamasisha usindikaji wa mazao badala ya kuyauza yakiwa ghafi.

Alisema waoneshaji zaidi ya 100 walitoa elimu ya vitendo kwa wananchi kupitia teknolojia mpya za uzalishaji, huku wafanyabiashara wakibadilishana mawasiliano yaliyofungua fursa mpya za biashara.

Luvanda alibainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo, mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji mdogo wa mitaji vinaendelea kuwa changamoto kubwa kwa wakulima, akisisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Mhandisi David Munkyala, alisema taasisi hiyo inaendelea kuwekeza katika tafiti za maji ya chini ya ardhi, uchimbaji wa visima na usimamizi wa matumizi ya maji ili kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinakuwa suluhisho la kudumu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema bodi hiyo pia inaendelea kutoa vibali vya matumizi ya maji kwa wakulima baada ya kufanya tathmini ya kitaalamu ili kuhakikisha matumizi hayo hayaathiri watumiaji wengine wala uendelevu wa vyanzo vya maji.

Maonesho ya mwaka huu yaliwakutanisha waoneshaji 101 kutoka taasisi za umma na binafsi, kampuni za pembejeo, wakulima, wafugaji, wavuvi, taasisi za fedha na wajasiriamali, huku wananchi wakipata fursa ya kujifunza teknolojia mpya, kufanya biashara na kujenga ushirikiano unaotarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi mkoani Iringa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *