WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema maendeleo ya kudumu ya Taifa hayawezi kupatikana bila kujenga wananchi wenye maadili, uzalendo, uwajibikaji na mshikamano, sambamba na kuendelea kuimarisha utawala wa sheria na taasisi za umma.

Akizungumza jijini  Dar-es-salaam wakati   alipokutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku, Dk Mwigulu  amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kujenga tabia njema za wananchi na kuimarisha taasisi ili kuhakikisha msingi imara wa maendeleo ya Taifa unaendelea kuimarika.

“Nchi haiwezi kupata maendeleo ya kudumu bila kuwa na wananchi wenye maadili, uzalendo na uwajibikaji. Tunapaswa kuendelea kujenga tabia njema za wananchi na kuimarisha taasisi zetu ili ziwe nguzo ya maendeleo,” alisema. SOMA: Butiku:Muungano sio wa viongozi ,Vyama vya Siasa

Kwa upande wake, Mzee Butiku amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake na juhudi anazoendelea kuzifanya katika kuiongoza nchi.Pia alimpongeza Waziri Mkuu kwa mchango wake katika kusimamia shughuli za Serikali na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali unaendelea kwa ufanisi.

Amesema amekuwa akifuatilia ziara za Waziri Mkuu katika mikoa mbalimbali na kushuhudia namna zilivyochangia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma. Aidha, Mzee Butiku  ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, ikiwemo kuitambua kama mshirika wa maendeleo ya Taifa na kuwezesha upatikanaji wa eneo la ujenzi wa Mwalimu Nyerere World Leadership Institute.

Vilevile amesisitiza umuhimu wa kuendelea kujenga jamii inayozingatia maadili, uzalendo, utawala wa sheria, haki za watu na misingi ya demokrasia.Amesema baadhi ya vitendo vya kuwavunjia heshima viongozi, wazee, viongozi wastaafu na viongozi wa dini havijengi utaifa na vinapaswa kuepukwa. Mzee Butiku  amewahimiza Watanzania kuendelea kukosoana kwa hoja na kwa kuzingatia sheria, huku kila mmoja akitimiza wajibu wake kwa lengo la kuimarisha amani, usalama, umoja na mshikamano wa Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *