Tanga. Baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) kutoka Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, wamemtaka Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha zinazomkabili, huku wakisema wanaweza kuandaa maandamano endapo hawatapata majibu kuhusu suala hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, Julai 20, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Tanga na viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bavicha Jimbo la Lushoto, Mambo Nkuya, Mwenyekiti wa Bawacha Jimboni humo, Gorda Ramadhani, pamoja na Katibu wa Chadema Jimbo la Handeni Mjini, Kombo Matulu.

Viongozi hao wamesema wanachama wa ngazi za chini wamekuwa wakihoji kuhusu tuhuma hizo, jambo ambalo limewaweka katika wakati mgumu kutokana na kukosa majibu rasmi kutoka kwa uongozi wa juu wa chama.

Nkuya amesema kwa mtazamo wao, hatua ya kiongozi anayetajwa katika tuhuma hizo kupisha uchunguzi inaweza kusaidia kurejesha imani ya wanachama.

“Tunapokutana na wanachama tunaulizwa maswali mengi kuhusu madai haya, lakini hatuna majibu. Tunaona kupisha uchunguzi kunaweza kuwa hatua ya busara,” amesema.

Pia amemtaka Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Tundu Lissu, kuachiwa huru, akisema anaamini uwepo wake ungeweza kusaidia kushughulikia changamoto zinazojitokeza ndani ya chama.

Kwa upande wake, Gorda Ramadhani amesema hawawezi kuthibitisha iwapo tuhuma zinazotolewa ni za kweli au la, akisisitiza umuhimu wa kufanyika kwa uchunguzi huru.

“Hatusemi madai haya ni ya kweli au si ya kweli. Tunachotaka ni uchunguzi ufanyike ili ukweli ujulikane,” amesema.

Aidha, amesema yuko tayari kuwajibika kwa kauli zake, lakini ameomba taratibu za chama zifuatwe iwapo hatua zozote za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Naye Kombo Matulu amesema baadhi ya wanachama wamekuwa wakifikiria kufanya maandamano wakidai kukosekana kwa majibu ya moja kwa moja kuhusu tuhuma hizo.

Amesema viongozi wa chama wanapaswa kushughulikia suala hilo kupitia utaratibu wa ndani wa chama ili kuondoa sintofahamu miongoni mwa wanachama.

Heche alivyowahi kujibu

Julai 17, 2026, akizungumza na wazee wa Chadema wilayani Tarime, Heche alisema madai yanayoelekezwa kwake hayawezi kumzuia kutekeleza majukumu yake ndani ya chama.

Alisema anaendelea kutekeleza maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema, ikiwemo kampeni za “Free Tundu Lissu” na “Katiba Mpya”, akisisitiza kuwa hataondolewa kwenye msimamo huo.

“Mimi ni dhahabu, siwezi kuchafuka,” alisema Heche.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *