Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imebadili mkakati wa kuimarisha huduma za afya kwa kuweka msisitizo katika ufuatiliaji wa karibu wa huduma zinazotolewa katika vituo vya afya, hatua inayolenga kupunguza vifo vya mama na watoto vinavyoweza kuzuilika.

Hatua hiyo imetangazwa leo, Jumatatu Julai 20, 2026, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mngereza Miraji Mzee, wakati wa hafla ya kukabidhi magari matano yenye thamani ya Sh750 milioni yaliyotolewa kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia.

Dk Mngereza amesema Serikali imeanzisha utaratibu mpya wa ufuatiliaji wa huduma za afya unaolenga kuongeza uwajibikaji wa watumishi pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi, hususan kwa wajawazito na watoto.

“Serikali imeamua kubadili mfumo wa ufuatiliaji wa huduma za afya kwa kuanzisha utaratibu mpya unaolenga kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma, hususan kwa wajawazito na watoto,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mngereza, magari hayo yatatumika na timu maalumu za Wizara ya Afya kufanya ziara za mara kwa mara katika wilaya na mikoa yote ya Zanzibar ili kufuatilia utoaji wa huduma na kuhakikisha viwango na miongozo ya sekta ya afya vinafuatwa.

Amesema tofauti na utaratibu wa awali, timu hizo zitafika moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa lengo la kubaini changamoto zinazojitokeza na kuzitatua kwa wakati kabla hazijasababisha madhara.

“Serikali imewekeza zaidi katika eneo hili ili timu zetu zifike moja kwa moja kwenye maeneo ya kutolea huduma kufuatilia utekelezaji na kushughulikia changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto,” amesema.

Dk Mngereza amesema baadhi ya magari hayo yamekabidhiwa kitengo cha afya ya mama na mtoto, ambacho kuanzia mwaka huu wa fedha kitapewa jukumu la kufanya ufuatiliaji wa karibu wa kila tukio la kifo cha mama au mtoto ili kubaini chanzo chake na kupendekeza hatua za kuzuia matukio kama hayo kujirudia.

“Kwa utaratibu huu, kila wiki tutakuwa tunapokea taarifa kutoka kwa timu zetu kuhusu changamoto mbalimbali zinazochangia vifo vya mama na mtoto ili wizara ichukue hatua stahiki kwa wakati,” amesema.

Amesema mfumo huo mpya unatarajiwa kuimarisha usimamizi na kuboresha huduma za afya, pamoja na kuongeza uwajibikaji wa watumishi katika ngazi zote za mfumo wa afya.

“Tunaamini uwekezaji huu utasaidia kupunguza vifo vinavyozuilika vya mama na watoto wachanga na kuimarisha huduma za afya ya uzazi na mtoto, ambalo ni eneo la kipaumbele kwa Serikali,” amesema.

Akizungumzia uwekezaji wa Serikali katika sekta ya afya, Dk Mngereza amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita zaidi ya Sh130 bilioni zimeelekezwa kwenye ujenzi wa hospitali 10 za wilaya, Hospitali ya Mkoa wa Lumumba, pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.

Amesema Serikali imepanga kuwekeza zaidi ya Sh1 trilioni katika sekta hiyo ifikapo mwaka 2030, huku utekelezaji wa mpango huo ukiwa tayari umeanza kupitia ujenzi wa hospitali nne za mikoa zilizobaki na Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Binguni.

Kwa upande wake, Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Afya Pemba, Khamis Bilal Ali, amesema magari hayo yataongeza uwezo wa wataalamu wa afya kufuatilia huduma na kutekeleza shughuli za mradi wa kupunguza vifo vya mama na mtoto unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

“Tunashukuru kupata magari haya ambayo yataimarisha utoaji wa huduma na kusaidia kufikia malengo ya kupunguza vifo vya mama na mtoto, hususan katika Kisiwa cha Pemba,” amesema.

Naye Meneja wa Kitengo Shirikishi cha Afya ya Uzazi na Mtoto, Dk Kamilia Ali Omar, amesema magari hayo yatawezesha wataalamu wa kitengo hicho kufanya ufuatiliaji wa huduma za afya ya mama, mtoto na lishe katika vituo mbalimbali vya afya.

Amesema pia yataimarisha ukusanyaji wa takwimu na ufuatiliaji wa ubora wa huduma, hatua itakayowezesha wizara kufanya uamuzi sahihi wa kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto.

“Tunaamini magari haya yatatuwezesha kufuatilia kwa karibu ubora wa huduma za afya ya mama na mtoto, pamoja na kupata takwimu sahihi ambazo ni msingi muhimu wa kupanga na kuboresha huduma,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *