
Dar es Salaam. Baada ya miaka kadhaa ya kusoma na kujenga matumaini ya maisha mapya, maelfu ya wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini wanaanza safari ya kuondoka rasmi vyuoni na kuingia katika hatua nyingine ya maisha.
Kwa mujibu wa kalenda za vyuo mbalimbali, mitihani ya mwisho imeanza wiki iliyopita na walioko miaka ya mwisho ya masomo yao wakijiandaa kurejea uraiani kukutana na uhalisia wa maisha nje ya vyuo.
Wengi wanabeba matumaini ya kupata ajira, kujitegemea na kutumia taaluma walizosomea, lakini wanakutana na soko la ajira lenye ushindani mkubwa kuliko walivyotarajia.
Takwimu za Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha kiwango cha ukosefu wa ajira kilishuka kutoka asilimia 8.9 mwaka 2023 hadi asilimia 6.2 mwaka 2024.
Hata hivyo, zaidi ya asilimia 90 ya ajira nchini bado zinapatikana katika sekta isiyo rasmi, hali inayoonesha kuwa fursa za kujipatia kipato zipo, lakini si zote ni ajira rasmi ambazo wahitimu wengi huzitarajia wanapomaliza masomo.
Baada ya kuhitimu, baadhi ya vijana huingia katika biashara ndogondogo kama umachinga, udalali, ujasiriamali wa bidhaa mbalimbali au shughuli nyingine za kibiashara ili kujipatia kipato wakati wakisubiri ajira rasmi.
Wengine huamua kuingia kwenye kilimo au kuanzisha shughuli za uzalishaji, hasa maeneo ya vijijini, huku wengine wakijikuta wakifanya kazi ambazo awali hawakuzifikiria, ikiwemo kuendesha bodaboda.
Mfano ni James Ndoni, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Mwanza, mwaka 2020, ambaye baada ya kumaliza masomo aliingia katika kazi ya kuendesha bodaboda kwa zaidi ya miaka mitatu kutokana na kukosa ajira inayolingana na taaluma yake ya ualimu.
Anasema baada ya kuhitimu alijaribu kutafuta nafasi mbalimbali za kazi, lakini kutokana na ushindani mkubwa katika soko la ajira alilazimika kutafuta njia nyingine ya kujipatia kipato.
“Nilikamilisha masomo yangu nikiwa na matumaini ya kupata kazi inayohusiana na taaluma yangu, lakini hali ya ajira ilinilazimisha kufanya uamuzi mwingine. Kuendesha bodaboda kumenisaidia kuendelea na maisha wakati nikiendelea kutafuta fursa nyingine,” anasema Ndoni.
Wapo pia baadhi ya wahitimu wanaoingia kwenye michezo ya kubashiri (kubeti), wakitumaini kupata kipato cha haraka kutokana na ugumu wa kupata ajira au mitaji ya kuanzisha biashara.
Hata hivyo, hali hiyo imekuwa ikizua mjadala kuhusu namna baadhi ya vijana wanavyotafuta njia mbadala za kuishi baada ya kumaliza masomo.
Kwa kundi jingine, baadhi hubaki wakiishi kwa utegemezi kwa wazazi, walezi au ndugu huku wakisubiri nafasi za ajira serikalini au sekta binafsi. Wengine hukaa mitaani na vijiweni wakisubiri taarifa za michongo ya kazi, mafunzo au fursa mbalimbali.
Katika mazingira hayo, baadhi ya wahitimu hukumbana na changamoto ya mawakala wa mitandao ya ajira (mawinga) wanaotumia hali hiyo kuwalenga kwa kuwaahidi kuwaunganisha na waajiri kupitia makundi mbalimbali ya mitandao, huku wakidai malipo ya usajili au ada za huduma.
Kunani kwenye familia?
Kwa upande wa familia zinazosomesha, changamoto ya ajira kwa wahitimu pia huongeza mzigo kwa wazazi waliowekeza fedha, muda na nguvu kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya juu.
Rehema Mashishanga, mzazi kutoka Mkoa wa Tabora, anasema baada ya binti yake kumaliza mitihani ya mwisho mwezi huu, matarajio yake makubwa ni kuona anapata kazi na kuanza kunufaika na elimu aliyopata.
“Tumepitia mengi kuhakikisha mtoto anafika hapa. Sasa matumaini yangu ni kuona anapata kazi ili mzigo wa kumhudumia upungue na sisi wazazi tuanze kuona faida ya elimu yake,” anasema.
Hali hiyo inaonesha kuwa safari ya wahitimu baada ya chuo hutofautiana. Baadhi hupata ajira rasmi, wengine hujiajiri, wengine huingia katika sekta isiyo rasmi, huku wengine wakisubiri kwa muda mrefu fursa ya kutumia elimu waliyoipata.
Wanayokutana nayo uraiani
Enock Bulai, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Mwanza, mwaka 2020, anasema matumaini aliyokuwa nayo alipokuwa akisoma yalibadilika baada ya kuingia mtaani, kwani hali aliyokutana nayo ilikuwa tofauti na matarajio yake.
Anasema aliamini kuwa baada ya kumaliza chuo angekuwa na nafasi nzuri zaidi ya kupata ajira kutokana na elimu aliyokuwa nayo, lakini hali hiyo haikutimia kwa miaka yote hadi sasa, jambo lililomlazimu kutafuta njia nyingine za kuishi bila kutumia taaluma yake.
“Tatizo ukimaliza chuo unakuwa mtu mzima, huwezi kupiga simu kwa mama kuomba vocha. Halafu unajiona una elimu, unachagua kazi za kufanya. Ukikutana na ugumu wa mtaani, kuna muda unafika unaweka pembeni taaluma yako, unafanya kazi yoyote ili upate kipato,” anasema.
Enock anawashauri vijana wanaomaliza vyuo kuingia uraiani wakiwa tayari kukabiliana na mazingira tofauti na kuwa tayari kufanya kazi mbalimbali wakati wakitafuta fursa zinazolingana na taaluma zao.
“Tangu nimalize chuo miaka sita sasa sijawahi kuajiriwa popote. Nimekuwa napeleka vyeti sehemu mbalimbali, naishia kuambiwa ‘not selected for oral interview’. Naendelea kupambana mtaani. Nimefanya kazi mbalimbali, ikiwemo kilimo, uchimbaji madini na biashara,” anaeleza.
Matarajio ya wahitimu
Pamoja na changamoto hizo, wahitimu wengi bado wana matumaini ya kutumia elimu yao kujenga maisha bora na kujitegemea.
Arafati Alli, mwanafunzi wa Sayansi ya Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema anatamani kuona elimu anayopata ikimsaidia kuingia katika soko la ajira, kuanza kujitegemea na kusaidia familia yake.
“Matumaini yangu baada ya kumaliza chuo ni kupata nafasi itakayoniruhusu kutumia ujuzi wangu wa kompyuta. Nikianza kupata mshahara nitakuwa na uwezo wa kujijenga na kusaidia wazazi wangu,” anasema Alli.
Kwa upande wake, Yasir Urasa, anayehitimu Shahada ya Uandishi wa Habari katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema anatamani kupata ajira itakayolingana na taaluma yake ili aanze kujenga maisha ya kujitegemea.
“Matarajio yangu baada ya kumaliza masomo yangu chuoni ni kupata ajira ambayo itaendana na nilichokisomea,” anasema.
Hamis Bakari, anayehitimu Shahada ya Ualimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema anatarajia kuanza kwa kupata kituo cha kufundishia ili kujenga uzoefu, huku akipanga baadaye kuanzisha biashara ya vifaa vya shule na kujiendeleza kitaaluma.
“Nataka kwanza nipate kituo cha kufundisha cha aina yoyote ili nipate nafasi ya kufanya mazoezi ya taaluma yangu, kisha nitajiendeleza kadiri ninavyopata fursa zaidi,” anasema.
Kwa upande mwingine, Monica Lukanda anaamini safari ya baada ya chuo inahitaji uvumilivu, kujifunza na kuongeza ujuzi badala ya kutegemea cheti pekee.
“Chuoni unajifunza nadharia, lakini mtaani unajifunza maisha. Cheti kinakufungulia mlango, lakini nidhamu, ujuzi na uvumilivu ndiyo vitakavyokufikisha mbali,” anasema.
Tofauti na wenzake wanaolenga kuajiriwa, Asha Mohamed anasema ameelekeza nguvu zake katika ubunifu wa maudhui, shughuli za kijamii na kilimo, akiamini kujiajiri kunaweza kuwa njia ya kutengeneza fursa kwa wengine.
“Nimebuni kitu kinacholenga kusaidia vijana wenye mawazo na ndoto ambazo wamekosa watu wa kuwashika mkono,” anasema.
Juhudi za Serikali
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali, huku Rais Samia Suluhu Hassan akisisitiza kuwa tatizo la ajira kwa vijana haliwezi kutatuliwa na Serikali pekee.
Anasema suluhisho linahitaji uwekezaji, kuimarisha sekta binafsi, kukuza ujuzi na kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri kupitia ujasiriamali na ubunifu.
Msisitizo huo unaendana na ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza fursa za ajira na kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za uzalishaji.
Aidha, Serikali inaendelea kuweka mkazo katika elimu ya ujuzi na kuboresha mfumo wa Vyuo vya Ufundi Stadi (Veta) ili kuwajengea uwezo wahitimu kujiajiri.
Pamoja na jitihada hizo, wahitimu wengi wanaoingia uraiani bado hukutana na ushindani mkubwa wa ajira, huku baadhi wakilazimika kufanya kazi zisizohusiana na taaluma zao ili kujikimu.
Wengine hukaa miezi au hata miaka kadhaa bila kupata ajira rasmi, hali inayowafanya kuendelea kutegemea familia kwa muda mrefu kuliko walivyotarajia.
Kadhalika, ingawa baadhi ya waajiri huwapa nafasi wahitimu wapya, waajiri wengi sasa hawazingatii cheti pekee, bali huangalia pia uzoefu wa kazi, ujuzi wa ziada na uwezo wa kutatua changamoto.
Wadau wataja suluhisho
Wakati mjadala wa changamoto ya ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu ukiendelea nchini, wasomi wanapendekeza ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kujenga uchumi wenye uwezo wa kuzalisha ajira.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, anasema changamoto ya ajira kwa wahitimu si suala la Tanzania pekee, bali linakabili nchi nyingi zinazoendelea.
Anasema suluhisho linapaswa kuangalia kwa pamoja ubora wa elimu inayotolewa na uwezo wa uchumi kuwachukua wataalamu wanaozalishwa.
“Nilikuwa kwenye mkutano nchini Nigeria tukijadili suala hili. Mtu mmoja akauliza, tukiwaleta leo wahitimu 2,000 kutoka MIT, Stanford au Oxford hapa Tanzania, je, wote watapata ajira? Hakukuwa na jibu la moja kwa moja. Hapo ndipo tukagundua pamoja na kuboresha mitaala, lazima pia tujenge uchumi unaozalisha ajira,” anasema.
Anasema vyuo vikuu vina jukumu la kuzalisha wahitimu wenye maarifa na ujuzi, lakini haviwezi kuwa waajiri, hivyo taifa linapaswa kujenga viwanda na sekta za teknolojia zitakazohitaji wataalamu hao.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Nelson Boniface, alipozungumza katika maadhimisho ya 11 ya utafiti ya chuo hicho Juni mwaka huu, alisema hatua hiyo imeonesha mafanikio katika kuwawezesha wahitimu kujitegemea kiuchumi.
“Kupitia tafiti na ujuzi, wahitimu wetu wengi wameweza kujiajiri na zaidi ya 800 wameomba mikopo kwenye taasisi za fedha kutokana na biashara wanazofanya,” alisema na kuongeza kuwa hilo linaweza kuwa suluhisho la tatizo la ajira kwa wahitimu nchini.
Mhadhiri wa uchumi, Malcom Lambert, anasema Tanzania imekuwa ikiwekeza katika kuongeza idadi ya wahitimu, lakini ukuaji wa sekta zinazoweza kuwaajiri haujaenda kwa kasi inayolingana.
“Unaweza kuzalisha wahitimu wengi wenye ujuzi mzuri, lakini kama uchumi hauna viwanda, kampuni za teknolojia, taasisi za utafiti na sekta zinazohitaji utaalamu huo, changamoto ya ajira itaendelea kuwepo,” anasema.
Naye mtaalamu wa sera za elimu, Patric Msuya, anasema elimu inaweza kumwandaa mtu kuwa bora zaidi, lakini haiwezi kuunda ajira bila kuwepo kwa mazingira ya uwekezaji na ukuaji wa sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, mtaalamu wa maendeleo ya jamii, Hadija Mbando, anasema nchi inahitaji kuunganisha ujuzi wa ufundi na maarifa ya elimu ya juu ili kujenga uchumi unaoshindana.
“Hatuwezi kuwa taifa la mafundi pekee wala taifa la wasomi pekee. Tunahitaji mfumo unaounganisha ujuzi wa ufundi na maarifa ya juu ili kujenga uchumi unaoshindana,” anasema.