PAMBA Jiji imeendelea kuziba mapengo ya wachezaji wao waliondoka, tayari imemalizana na kiungo mkabaji John Ochieng  akitokea Zanaco FC ya Zambia aliyokuwa amejiunga nayo Agosti 23, 2023 ukiwa ni usajili wa kuziba pengo la kiungo Kelvin Nashon aliyejiunga na Simba.

Usajili wa Ochieng aliyezaliwa Desemba 15, 2003 (umri wa miaka 23) nchini Kenya, unakwenda kuziba pengo la kiungo huyo mkabaji aliyetambulishwa na klabu ya Simba kuwa sehemu ya kikosi chao msimu ujao unaoanza Agosti 14, 2026.

Kiungo huyo kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa Zambia, nchini kwao aliwahi kuzichezea Gor Mahia FC, Chemelil Sugar, Tusker FC pia na timu ya taifa ya vijana na wakubwa ya Harambee Stars.

Alipotafutwa kocha wa timu ya Pamba, Francis Baraza kuhusiana na usajili huo amesema:”Siwezi kuzungumzia usajili wa mchezaji mmoja mmoja kila mchezaji aliyepo Pamba ujue ni muhimu na anategemewa kutimiza malengo ya klabu.”

Ameongeza:”Tunatamani msimu ujao uwe wa mafanikio zaidi kwa Pamba, hilo ndilo jambo la msingi, naamini viongozi wanasajili wachezaji wenye uwezo wa juu.”

Ukiachana na kiungo huyo, Pamba pia ilimsajili golikipa Mkenya, Steve Ochieng kutoka Shabana FC ambaye ni mbadala wa Yona Amosi aliyekwenda kujiunga na Singida Black Stars, inayojiandaa kucheza michuano ya  Cecafa Kagame Cup yanayofanyika nchini Rwanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *