
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Afrika inapaswa kutumia mabadiliko yanayoendelea katika siasa, uchumi na usalama duniani kama fursa ya kuharakisha maendeleo yake.
Amesema bara hilo linapaswa kufanya hivyo kwa kuimarisha uongozi wa kimkakati, kuongeza thamani ya rasilimali zake na kujenga taasisi imara zitakazolinda masilahi ya wananchi wake na kuharakisha maendeleo.
“Afrika isiendelee kuwa uwanja wa ushindani wa mataifa makubwa. Tunapaswa kutumia nafasi yetu ya kimkakati, rasilimali tulizonazo na nguvu ya watu wetu kujiletea maendeleo yenye manufaa kwa wananchi wetu,” amesema.
Dk Mwgulu amesema hayo leo Jumanne, Julai 21, 2026 alipokuwa mzungumzaji mkuu katika Mkutano wa pili wa wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC) uliofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Amesema dunia inaendelea kushuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama yanayochochewa na ushindani wa mataifa makubwa, maendeleo ya teknolojia, mabadiliko ya nishati na ushindani wa rasilimali muhimu, hali inayozitaka nchi za Afrika kuwa na viongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi ya kimkakati kwa manufaa yake.
Amesisitiza Afrika ina takribani asilimia 30 ya madini muhimu yanayohitajika katika mapinduzi ya teknolojia na nishati safi duniani, hivyo Bara hilo linapaswa kutumia nafasi hiyo kujenga uchumi imara kupitia kuongeza thamani ya rasilimali zake badala ya kuendelea kuuza malighafi na kutegemea mataifa mengine.
“Afrika lazima iache kuwa uwanja wa ushindani wa mataifa makubwa. Tunapaswa kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya rasilimali zetu, kuimarisha biashara ndani ya Bara na kutumia fursa zilizopo kujenga uchumi shindani na endelevu,” amesisitiza.
Aidha, Waziri Mkuu amesema viongozi wa Afrika wanapaswa kujenga taasisi zenye uwezo wa kusimamia maendeleo, kulinda masilahi ya wananchi na kuhakikisha rasilimali za Bara zinatumika kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumzia hali ya usalama duniani, Waziri Mkuu amesema migogoro ya kimataifa imeendelea kuathiri uchumi wa Afrika kupitia kupanda kwa gharama za nishati, usafirishaji, bidhaa na huduma, hali inayosisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kujenga uchumi unaostahimili misukosuko ya nje, kuimarisha biashara baina ya nchi za Afrika na kuongeza ushirikiano wa kikanda.
Amesema changamoto hizo zinapaswa kuwa chachu ya Afrika kuwekeza zaidi katika viwanda vinavyoongeza thamani ya malighafi, teknolojia, utafiti na ubunifu ili kujenga uchumi imara na unaojitegemea.
Dk Mwigulu pia amewataka washiriki wa mkutano huo, ambao ni viongozi waandamizi kutoka sekta mbalimbali, kutumia jukwaa hilo kujadili na kutoa mapendekezo yatakayosaidia Afrika kubadili changamoto za kisiasa, kiuchumi na kiusalama kuwa fursa za maendeleo endelevu.
Awali, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, Meja Jenerali Wilbert Ibuge, amesema mkutano huo unalenga kuwakutanisha wahitimu wa chuo hicho ili kubadilishana uzoefu, kuimarisha mtandao wa viongozi wa kimkakati na kujadili masuala muhimu yanayohusu siasa, uchumi, uongozi na usalama kwa maendeleo ya Afrika.
Naye, Kansela wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, Dk Abdulhamid Mzee amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kitaaluma linalowakutanisha wahitimu, wataalamu na viongozi mbalimbali kwa ajili ya kujadili changamoto na fursa zinazolikabili Bara la Afrika katika mazingira ya sasa ya dunia.
Baada ya mzungumzaji mkuu kuwasilisha mada yake, mkutano uliendelea kwa mjadala wa kitaalamu kuhusu mwenendo wa siasa, uongozi, uchumi na usalama katika karne ya 21 pamoja na athari zake kwa maendeleo ya Afrika.
Mjadala huo uliowashirikisha wataalamu na viongozi mbalimbali akiwemo Profesa Rwekaza Mukandala, Balozi Ombeni Sefue, Profesa Adolf Mkenda (Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia), Kamanda wa Jeshi la Kenya na mhitimu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, Luteni Jenerali David Ketter pamoja na Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu).