
Mashambulizi ya Iran dhidi ya vituo vya Marekani nchini Jordan yanachukuliwa kuwa miongoni mwa operesheni zilizofanikiwa zaidi katika mzozo wa kijeshi wa hivi karibuni kati ya Iran na Marekani.
Mwezi huu wa Julai, Iran ilianzisha mfululizo wa mashambulizi makali dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko katika ardhi ya Jordan. Hali ya kuendelea kwa mashambulizi hayo, idadi ya wahanga walioathirika na udhaifu uliojitokeza katika mifumo ya ulinzi ya Marekani, ni ishara ya kuongezeka kwa kiwango kikubwa mzozo katika eneo hili nyeti la Asia Magharibi. Mashambulizi hayo ya Iran ni sehemu ya kampeni ya mashambulizi yanayotekelezwa katika hatua tofauti, makali yaliyopangwa kwa ustadi mkubwa na kufanywa kwa usahihi wa hali ya juu, yote yakitekelezwa ndani ya kipindi cha chini ya wiki moja.
Kwa mujibu wa ripoti za CENTCOM—ambayo kwa kawaida hupunguza uzito wa taarifa kuhusu vifo, majeruhi na uharibifu uliopatikana kwa vikosi vya Marekani, jeshi la Iran lilifanya mashambulizi manne makubwa katika kipindi cha siku tano, huku kila shambulio likionyesha kuongezeka kwa makali kulingana na walengwa na kiwango cha uharibifu.
Shambulio la kwanza lililenga kambi ya kijeshi ya Marekani katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Mfalme Faisal, na kusababisha majeraha kwa wanajeshi watano. Wimbi la pili la mashambulizi lililenga kambi moja mashariki mwa Jordan, likilenga zaidi vifaa vya kijeshi, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa helikopta kadhaa aina ya Black Hawk. Tukio la tatu lilitokea katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Muwaffaq Salti. Takriban wanajeshi 20 wa Marekani walijeruhiwa katika tukio hilo, ingawa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) ilidai kuwa hakukuwa na vifo.
Shambulio la nne na baya zaidi pia lilifanyika katika kambi hiyo hiyo ya Al-Salti. Mnamo tarehe 17 Julai, Iran ilitekeleza shambulio la mwisho na la nguvu kwa kutumia mchanganyiko wa makombora yanayolenga shabaha kwa usahihi wa hali ya juu na ndege zisizo na rubani. Shambulio hilo lililenga moja kwa moja maeneo yaliyokuwa na wanajeshi wa Marekani.
Mnamo tarehe 18 Julai, CENTCOM ilithibitisha kuwa wanajeshi wawili wa Marekani waliuawa, huku mmoja akitoweka, ambapo wengine wanne walijeruhiwa katika shambulio hilo. Baadaye, CENTCOM ilitangaza kupatikana kwa mabaki ya mwanajeshi huyo aliyekuwa ametoweka. Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa makombora hayo, mbali na kusafiri kwa kasi kubwa, hulibadili mwelekeo yanapokaribia shabaha iliyolengwa ardhini, na hivyo kufanikiwa kupenya mifumo ya ulinzi wa anga ya Wamarekani.
Mbali na vifo vya askari, kulikuwa na uharibifu mkubwa ilofanyika dhidi ya zana za kijeshi za adui. Kuhusu shambulio la Julai 16, Iran ilitangaza kwamba ilishambulia Kituo cha Anga cha Muwaffaq Salti, ikilenga mfumo wake wa rada, mtandao wa mawasiliano na vituo vya mafuta. Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) baadaye lilisema kwamba shambulio la Julai 18 kwenye kituo hicho liliharibu ndege zisizopungua tano za kivita. Taarifa ya baadaye ya IRGC mnamo Julai 21 ilisisitiza kwamba kombora lake liliharibu mfumo wa rada ya ulinzi wa anga katika kituo cha Marekani huko Jordan na kuharibu ndege ya kivita aina ya F-15E ndani ya maegesho ya ndege.
Katika mashambulizi ya hivi karibuni ya makombora ya Iran, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Hussein katika mji wa Aqaba ulipigwa kwa makombora kadhaa. Picha zilizosambazwa zinaonyesha moshi mkubwa mweusi ukipaa angani kufuatia athari za makombora ya balistiki ya Iran, jambo linaloashiria kuwa makombora hayo yalilenga maeneo ya kijeshi yaliyokusudiwa katika uwanja huo wa ndege. Kwa sasa, idadi kubwa ya ndege za kijeshi za Marekani zimehamishiwa kwenye uwanja huo kutoka kambi za Marekani katika Ghuba ya Uajemi, ikiwa ni pamoja na ndege za doria ya baharini aina ya P-8A na ndege za uchukuzi aina ya C-17 na C-130 za Jeshi la Anga la Marekani.
Kwa mujibu wa CENTCOM, kufikia tarehe 19 Julai, jumla ya vifo vya Wamarekani vilikuwa vimefikia 16, huku idadi ya majeruhi ikiwa ni 427.
Mashambulizi ya Iran dhidi ya Jordan yamekuwa na matokeo makubwa. Makombora ya Iran yalivuruga juhudi zote za Jordan za kujaribu kuficha uwepo wa kambi za kijeshi za Marekani katika ardhi yake, kambi ambazo zilianzishwa kwa usiri mkubwa. Zaidi ya hayo, mashambulizi hayo ya makombora yamelenga maeneo yaliyo ndani ya ardhi ya Jordan badala ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, jambo linaloashiria kuwa, katika hatua hii, Jordan imeongezwa kwenye orodha ya Iran ya maeneo yanayolengwa, ikibadilika kutoka kuwa eneo la kupitishiwa makombora tu na kuwa shabaha halisi.
Kwa mtazamo wa kijeshi, mashambulizi haya yamefichua udhaifu mkubwa katika mifumo ya Marekani ya kuzuia makombora pale inapokabiliwa na mashambulizi ya makombora mengi kwa wakati mmoja pamoja na teknolojia mpya ya makombora ya Iran. Mafanikio makubwa ya mashambulizi ya Iran katika medani ya vita dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi za Kiarabu yameibua hofu na wasiwasi mkubwa kwa makamanda wakuu wa Marekani.
Kwa upande wa kisiasa, mashambulizi haya makali ya Iran yamemwacha Rais wa Marekani, Donald Trump, katika njia panda na kumfanya atishie eti kutoa “majibu makali zaidi” dhidi ya Iran. Wachambuzi wanaamini kuwa Iran imeratibu mashambulizi yake kwa lengo la kuongeza gharama za kisiasa kwa washirika wa Marekani katika eneo, na hivyo kutoa changamoto kwa nchi za Kiarabu zilizo na kambi za kijeshi za Marekani na kuzilazimisha zitazame upya mahesabu yao ya kimkakati.