
Tanga. Sakata la matumizi ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange mkoani Tanga limechukua sura mpya baada ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Jumuiya ya Wafanyabiashara Wadogo Tanzania (JWT) na Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kusisitiza kuwa hawajakataa kukitumia kituo hicho.
Badala yake, wadau hao wamependekeza utaratibu wa sasa uendelee kwa muda wa miezi sita ili wamiliki wa mabasi wasiokuwa na vituo vyao vya kisasa (terminal) wajenge, huku Halmashauri ya Jiji la Tanga ikitakiwa kufanya maboresho katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange ili kiwe rafiki zaidi kwa abiria.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kupendekeza kituo hicho kibadilishwe matumizi na kuwa maegesho ya malori iwapo mpango wa kuhamishia mabasi yote kuanzia safari zake katika eneo hilo utaendelea kukwama.
Mapendekezo hayo yalitolewa jana, Alhamisi, Julai 23, 2026, baada ya kamati hiyo kutembelea stendi hiyo na kujadili hatima yake kufuatia kusuasua kwa utekelezaji wa uamuzi wa kuhamishia huduma za mabasi katika kituo hicho.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Meya wa Jiji la Tanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uongozi, Mustapha Muhina maarufu Selebosi, alisema kamati imesikitishwa na kusimama kwa jitihada za kuanza matumizi kamili ya kituo hicho licha ya Serikali kuwekeza fedha nyingi kukijenga.
Alisema halmashauri ilikuwa ikitekeleza maelekezo ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) yaliyozitaka halmashauri kutumia vituo vikuu vya mabasi kwa mujibu wa sheria, lakini baadaye ikaelekezwa kusitisha utekelezaji huo na kuruhusu mabasi kuendelea kupakia na kushusha abiria katikati ya jiji.
Kauli ya wadau
Hata hivyo, leo Ijumaa, Julai 24, 2026, viongozi wa Taboa, JWT na TCCIA walikanusha madai kuwa wamegoma kutumia Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange.
Wakizungumza na waandishi wa habari, walisema mabasi yote yaendayo mikoani yamekuwa yakipitia katika kituo hicho kabla ya kuendelea na safari zake, hivyo si sahihi kusema wamekataa kukitumia.
Makamu Mwenyekiti wa Taboa Mkoa wa Tanga, Albert Peter, amesema wao pamoja na wananchi wameshtushwa na taarifa za kubadilishwa matumizi ya kituo hicho, huku wakisisitiza kuwa hawajawahi kupinga matumizi yake.
Amesema walikubaliana na uongozi wa halmashauri kuwa kabla ya kituo hicho kuanza kutumika kikamilifu yafanyike maboresho muhimu, ikiwamo kuwekwa viti vya abiria, huduma ya kwanza, kituo cha polisi na kuboreshwa kwa kituo cha daladala.
“Tulikubaliana na halmashauri kuwa maboresho hayo yafanyike kwanza, lakini hadi sasa hayajatekelezwa,” amesema.
Meneja wa TCCIA Mkoa wa Tanga, Charles Hoza, amesema taasisi hiyo imeamua kuingilia kati baada ya Taboa na JWT kuomba kufanyika kwa mazungumzo yatakayowezesha kupatikana kwa suluhu ya kudumu.
Naibu Katibu wa Taboa Mkoa wa Tanga, Hassan Hashim, amesema chanzo cha sintofahamu hiyo ni uamuzi wa halmashauri kupiga marufuku mabasi kupakia abiria katika terminal zao zilizopo katikati ya mji na kuagiza safari zote zianzie Kange.
Hashim amesema wamiliki wa mabasi hawajawahi kupinga agizo hilo kwa sababu magari yao yanapitia Kange, kulipa tozo zote zinazotakiwa na kukaguliwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).
“Hatukuwahi kukataa kutumia Kange. Mabasi yetu hupitia hapo, hulipa tozo zote na kukaguliwa kabla ya kuendelea na safari. Tumeshangazwa kusikia kwamba tumegoma kutumia kituo hicho, jambo ambalo si kweli,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa JWT Mkoa wa Tanga, Ismail Masoud, amesema baada ya mazungumzo kati ya wafanyabiashara na wamiliki wa mabasi walikubaliana kuomba kupewa miezi sita ili wamiliki ambao hawana terminal wajenge.
Amesema katika kipindi hicho halmashauri itumie muda huo kuboresha huduma katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange ili kiwe tayari kutoa huduma bora kwa wasafiri.
“Tunapendekeza kwa miezi sita utaratibu wa sasa uendelee. Baada ya kipindi hicho, basi lolote lisitumie tena barabara za mjini kupakia au kushusha abiria. Kila mmiliki awe na terminal yake, na ambaye hatakuwa nayo aanzie safari zake Kange. Watakaokiuka wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema.
Selebosi atetea msimamo
Mwananchi limezungumza na Muhina (Selebosi) kuhusiana na uamuzi wa kutaka mabasi yaanzie safari Kange. Amesema ulifikiwa baada ya vikao vilivyowahusisha wamiliki wa mabasi, Latra na Jeshi la Polisi.
Amesema halmashauri ilitumia hata gari la matangazo kuhamasisha wananchi kuhusu kuanza kwa utaratibu huo kuanzia Julai 15, lakini siku ya utekelezaji ilielekezwa kusitishwa bila ushirikishwaji wa halmashauri.
“Tulikubaliana na wadau wote, tukatangaza rasmi kuwa kuanzia Julai 15 mabasi yote yaendayo mikoani yaanzie Kange. Lakini siku ya kuanza utekelezaji, maagizo hayo yalisitishwa ghafla bila sisi kushirikishwa,” amesema.
Amesema haoni busara kwa kituo hicho kuendelea kutotumika kama kilivyokusudiwa wakati Serikali imewekeza fedha nyingi kukijenga pamoja na jengo la kitega uchumi lenye huduma mbalimbali kwa wananchi.
“Lengo la Serikali lilikuwa wananchi wanufaike na kituo hiki pamoja na kuongeza mapato ya jiji. Hakitakiwi kubaki bila kutumika kama kilivyokusudiwa,” amesema.