
Dar es Salaam. Mitandao ya watu wanaoratibu na kuendesha udanganyifu wa mitihani nchini imewekwa kwenye rada za Serikali, huku wahusika wakionywa kuwa hatua kali zitaendelea kuchukuliwa ili kulinda uadilifu wa mfumo wa elimu.
Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ikiwa ni siku chache baada ya Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kutoa matokeo ya mtihani wa Kidato cha Sita, ambapo wanafunzi 58 walifutiwa matokeo kwa sababu ya udanganyifu, ikiwemo matumizi ya Akili Unde.
Profesa Mkenda amesema watu wanaoendesha na kuratibu mifumo ya udanganyifu wa mitihani wajiandae kukabiliana na mkono wa sheria, kwani Serikali haitavumilia mtandao wowote unaohujumu uadilifu wa mfumo wa elimu nchini.
“Hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wote wanaohusika na udanganyifu wa mitihani, iwe ni katika shule za umma au binafsi. Lengo ni kulinda ubora wa elimu badala ya kuwakandamiza wawekezaji. Hatufanyi hivyo kwa sababu tunachukia uwekezaji, bali tunalinda uadilifu wa elimu yetu,” amesema.
Amesema Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kudhibiti uvujaji wa mitihani na vitendo vya udanganyifu kupitia hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika miaka ya karibuni, ingawa bado kuna changamoto zinazohitaji kuendelea kushughulikiwa.
“Tumefanikiwa kwa asilimia kubwa sana kudhibiti uvujaji wa mitihani na udanganyifu. Sasa hivi tuko vizuri kweli kweli, lakini bado tutaendelea kuchukua hatua,” amesema.
Profesa Mkenda amesema matumizi ya simu za mkononi na teknolojia ya Akili Unde yameibua mbinu mpya za udanganyifu. Ndiyo maana kanuni za mitihani zinakataza mtahiniwa kuingia na kifaa chochote cha kidijitali au kuunganishwa mtandaoni wakati wa mtihani.
Kwa upande wa walimu, amesema watakaobainika kushiriki kusaidia udanganyifu wa mitihani hawatasalimika, akieleza kuwa Serikali inaendelea na maandalizi ya mfumo wa leseni kwa walimu wote nchini.
“Mwalimu tukijua unasaidia udanganyifu, kazi huna. Tukishaanza mfumo wa leseni za walimu, tutachukua leseni ya anayebainika kufanya udanganyifu na hataruhusiwa kufundisha tena,” amesema.
Waziri huyo amelipongeza Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Mtendaji Mkuu wake na walimu wanaosimamia mitihani kwa kazi ya kuimarisha usimamizi wa mitihani na kupunguza kwa kiwango kikubwa vitendo vya udanganyifu.
Aidha, amewataka wazazi kuhakikisha watoto wao hawaendi kwenye vyumba vya mitihani wakiwa na simu, akisisitiza kuwa hata mwanafunzi aliyeingia na simu bila kuitumia anaweza kufukuzwa kwa mujibu wa kanuni.
“Unaweza ukawa umejisahau ukaingia na simu, lakini tukikukamata tunakufukuza. Hatutaki kuzalisha wahitimu waliopata sifa kwa udanganyifu,” amesema.
Profesa Mkenda amesema matumizi ya Akili Unde yataendelea kuhamasishwa katika kujifunza na kufundishia, lakini yatumike kwa kuzingatia maadili na si kama njia ya kufanya udanganyifu.
“Fikiria unaenda kutibiwa na daktari aliyefaulu kwa kudanganya kwenye mitihani. Hilo ndilo tunalopambana nalo ili kuhakikisha wahitimu wetu wana ujuzi wa kweli,” amesema Profesa Mkenda.
Akizungumzia hilo, mtaalamu wa sera za elimu, Daniel Mathew, amesema udanganyifu wa mitihani haupaswi kupambanwa nao kwa adhabu pekee, bali pia kushughulikia sababu zinazowasukuma baadhi ya wanafunzi kutafuta njia hizo.
Amesema baadhi ya changamoto kama presha ya kupata alama kubwa, ushindani wa shule na matarajio ya wazazi vinaweza kuwafanya baadhi ya wanafunzi kutumia mbinu zisizo sahihi.
“Ni muhimu kujenga utamaduni wa kuthamini maarifa na uwezo halisi wa mwanafunzi kuliko kuangalia matokeo pekee,” amesema Mathew.