
Dar es Salaam. Madai ya Katiba mpya nchini Tanzania yamepata msukumo mpya baada ya Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi kuwataka Watanzania ‘kukomaa’ wapate Katiba mpya, suala lililowakuna wadau wa demokrasia na haki za binadamu.
Hatua hiyo ni baada ya Dk Nchimbi kuwataka wahakikishe hilo linafanyika kwa sasa, kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha utashi wa kutaka Katiba mpya, hivyo watumie fursa hiyo kuipata kwa kuwa anaweza kutokea Rais mwingine ambaye hana mpango nayo.
Dk Nchimbi amesema hayo jana Julai 24, 2026 katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), akieleza kuwa mchakato wa kupata Katiba mpya umechukua muda mrefu tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini sasa ni wakati sahihi wa kuendelea kuusukuma.
Wadau waeleza matumaini
Akizungumza baada ya hotuba hiyo, Naishorwa Masago kutoka Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC), alisema ameipokea kwa furaha kauli yake, akisema imetia matumaini ya kupatikana Katiba mpya.
“Hotuba ya Makamu wa Rais imefafanua mambo ya msingi ambayo yakitekelezwa yataimarisha ulinzi wa haki za binadamu. Inatia matumaini kuona viongozi wameona umuhimu wa kuungana na wananchi kuhitaji Katiba mpya itakayoweka misingi ya ulinzi wa haki za binadamu,” amesema.
Kwa upande wake, Hussein Wamaywa kutoka Umoja wa Wawezeshaji Kioo – Kigoma, amesema hotuba ya Makamu wa Rais inagusa masikio ya Watanzania walio wengi mbali na wanasiasa pekee, kwani kimekuwa kilio cha muda mrefu.
Amesema kauli yake kuhusu Katiba mpya imebeba maneno wanayotaka kusikia wananchi wa kawaida kuhusu ulinzi wa haki za binadamu nchini.
“Wasiwasi wangu kama mdau wa haki ni katika utekelezekaji wake kwani kauli nyingi zinazotolewa kwenye makongamano zimekuwa zikichukua muda mrefu bila utekelezekaji lakini kwakuwa amesema yeye hapa tunaamini itatimia,” amesema.
Kwa upande wake, Ombeni Kimaro kutoka Jukwaa la Haki za Mtoto Tanzania, amesema wito wa Makamu wa Rais kuhusu Katiba mpya umekuja wakati mwafaka, akisema yapo maeneo yenye upungufu, ambayo yanahitaji maboresho.
“Upo upungufu ambao tunautambua na tunatamani kuona mabadiliko. Lakini tunatamani Katiba mpya hiyo iwe na matokeo chanya kwenye ulinzi wa binadamu na yasipunguze hizo haki,” amesema.
Amefafanua kuwa mabadiliko ya Sheria mbalimbali yaliyofanyika miaka kadhaa hivi karibuni, hayakutoa nafasi nzuri kwa uhuru wa maoni, akisisitiza kuwa Katiba mpya iongeze uhuru na utetezi wa haki ya kutoa maoni.
“Pia, tunatamani Katiba mpya imtambue mtoto na haki zake, iongeze uhuru na haki ya watu kutoa maoni yao maana tunaona haki hiyo imefifia,” amesema.
Alichosema Dk Nchimbi
Ameeleza moja ya mambo muhimu katika safari ya kupata Katiba mpya ni uwepo wa utashi wa kisiasa kutoka kwa kiongozi mkuu wa nchi, akisisitiza kwamba kwa mfumo wa sasa wa uongozi, uamuzi mkubwa ya kitaifa unahitaji uamuzi wa Rais.
“Ningekuwa na njia ya kulifanya jambo hili bila hata Rais kutaka, ningewaambia Rais anaitaka (Katiba mpya) sukumeni, lakini mazingira hayaruhusu, inabidi usemee kwenye jukwaa.
“Kwa hiyo, hili Rais Samia anataka litekelezwe. Ni vizuri tukatumia fursa hii ambayo Rais analitaka likatekelezwa na Tume ya Haki Jinai aliyoiunda ilishauri lifanyike kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2029 na uchaguzi mkuu wa 2030,” amesema Dk Nchimbi.
Makamu wa Rais amesema Tume ya juzi ya Jaji Othman Chande (ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa Amani Oktoba 29, 2025) imesema Katiba mpya ipatikane kabla ya mwaka 2028 ili itumike katika uchaguzi wa 2029 na 2030.
“Komaeni hapo, tusisubiri aje Rais ambaye hataki Katiba mpya. Kwa Katiba iliyopo sasa Rais mbinafsi ataitaka tu kwa sababu inampa nguvu zisizo na maana.
“Tusiruhusu tupate Rais ambaye hana hamu na Katiba, tutaendelea kuitafuta Katiba mpya kwa miaka 50 mingine. Kwa kuwa Mama Samia kaonyesha ana nia, komaeni hapo hapo, niwaambie nini mwelewe?”
Vilevile, ameongeza kuwa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, zaidi ya 350 ambayo ameagiza yatekelezwe, kama yatatekelezwa, Tanzania haitabaki kama ilivyo sasa.
Amesema kuna mambo mengi ya ovyo yanafanyika, lakini Rais kasema mambo hayo yaondolewe.
“Viko vitu vingi, habari ya watu kukaa mahabusu kwa vikesi vidogodogo, vya kijingajinga, vingi tu; habari ya watu kukosa dhamana kwa vikosa vya kijingajinga tu,” amesema
Akitoa mfano, amesema: “Wapo watu wana roho mbaya tu, anajua kwamba wikendi huwezi kupata dhamana, kwa hiyo anakupeleka mahabusu Ijumaa jioni ili apate uhakika kwamba utakaa ndani siku mbili,” amesema.
Julai 2023, Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia iliwasilisha ripoti yake yenye mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuhuisha mfumo wa haki na kusisitiza kufuata sheria.
Dk Nchimbi amesema anachotaka Rais ni kuona watetezi wa haki za binadamu wanamuunga mkono, kwamba mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai yatekelezwe na Tanzania ikifika hapo itakuwa ni nchi nzuri na bora kuliko wakati mwingine wowote.
“Naomba mtoke hapa mkijua fursa tumeipata ya kupata Katiba mpya kabla ya mwaka 2030, kupata Katiba mpya ambayo itatumika katika uchaguzi wa 2019 na 2030. Narudia kusema tukomae hapo,” amesema.
Ameelekeza wito wake huo kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), vyama vya upinzani, asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu, kwamba Katiba mpya ni kwa faida ya watoto wao, wajukuu na vizazi vijavyo.
“Katiba mpya ni kwa faida ya nchi yetu, tupigane wote kupata Katiba mpya, tukishafika hapo kasi ya maendeleo na mabadiliko kwenye nchi yetu itakuwa kubwa kuliko mnavyofikiri,” amesema.
Amemnukuu Rais Samia wakati wa hotuba yake alipowaapisha majaji, Mei 2026, akisema, “haki ni msingi wa amani.”
Amesema baada ya hapo alimshukuru kwa kutamka maneno hayo hadharani ili kila kiongozi akayaeleze na kuyasimamia.
“Ukishaanza kuona haya kutamka ‘haki ni msingi wa amani’, unaanza kuona haya kutekeleza haki. Hakuna mashindano ya nani anaanza, haiwezekani mtetezi wa amani akawa adui wa haki au mtetezi wa haki akawa adui wa amani, ni jambo ambalo ni muhimu tujiepushe nalo,” amesema.
Amesema anatamani kuona kuna Tanzania ambayo kila Mtanzania anajisikia fahari kwa Utanzania wake, anajisikia amani ndani ya nchi yake, anajisikia yuko salama ndani ya nchi yake na kila Mtanzania ana hamu katika kuchangia maendeleo ya nchi yake.
“Natamani nchi ambayo tunatofautiana katika itikadi, tunatofautiana mambo ya vyama vya siasa, tunatofautiana mambo ya dini na makabila, lakini tunatambuana kwa Utanzania wetu, hii ndiyo nchi ninayoitamani.
“Natamani nikikutana na mwanaharakati yeyote yule, nimtambue kwa uwezo wake wa kufikiri na kushawishi…mtu akiniona nazungumza na Mariah Sarungi (mwanaharakati), anasema wanazungumza mambo ya nchi yao, wanakuwa na amani,” amesema.
Madai ya kihistoria
Kwa ujumla, hotuba ya Dk nchini, imeongeza pingili kwenye mnyororo wa madai ya muda mrefu ya Katiba mpya nchini Tanzania. Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Tume ya Jaji Francis Nyalali iliyoundwa na Rais Ali Hassan mwinyi ilipendekeza pamoja na kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi pia kutungwa kwa Katiba mpya, lakini pendekezo hilo halikutekelezwa.
Mwaka 1998, Rais Benjamin Mkapa aliunda Kamati ya Jaji Robert Kisanga kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba, huku mwanasiasa Christopher Mtikila akiendeleza mapambano mahakamani akidai mageuzi ya mfumo wa kisiasa na uchaguzi.
Mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, iliyokusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba. Hata hivyo, mchakato huo ulisimama mwaka 2014 baada ya Bunge Maalumu la Katiba kupitisha Katika iliyopendekezwa, huku kura ya maoni iliyotarajiwa ikishindikana.
Baadaye, Kamati ya Profesa Rwekaza Mukandala nayo zilitoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa uchaguzi na utawala na kuendeleza mchakati wa Katiba mpya.
Katika miaka ya karibuni, Tume ya Jaji Mohamed Chande ya Haki jinai na wadau mbalimbali wameendelea kusisitiza umuhimu wa mageuzi ya kisiasa na kisheria, huku madai ya Katiba mpya yakiendelea kuwa ajenda ya kudumu katika mijadala ya kitaifa.