Iran imekosoa vikali kauli za mkuu wa diplomasia wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran, huku ikibaki kimya kuhusu jinai za vita zinazofanywa na Marekani na Israel dhidi ya nchi hii, na kuzitaja kuwa ni “aina safi kabisa ya unafiki.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, ameandika hivi katika ujumbe wake kwenye akaunti yake ya X siku ya Jumamosi.

 “Je, kujidai kuwa mtetezi wa haki za binadamu kunawezaje kupatanishwa kwa urahisi kiasi hiki na kutoa msaada wa kiufundi na kiufundi-logistiki kwa mashambulizi ya mauaji dhidi ya wananchi wa Iran; mashambulizi yanayolenga kwa makusudi raia na miundombinu muhimu ya kitaifa?”

Ameongeza kuwa: “Na yote hayo huku wakikataa kulaani hata jinai za vita zilizo wazi kabisa, na bila kutoa hata neno moja la pole kwa watoto wa Iran waliouawa kwa mabomu na makombora ya Marekani na Israel yaliyoungwa mkono na ‘msaada wa kiufundi na kiufundi-logistiki’ wa EU yenyewe.”

Baghaei ameongeza kuwa hilo haliashirii tu “kupoteza itibari,” bali ni “uovu kamili na unafiki wa wazi.”

Mkuu wa sera za nje wa EU, Kaja Kallas, alisema siku ya Ijumaa kuwa umoja huo wa kisiasa na kiuchumi wa nchi 27 umeweka vikwazo vipya dhidi ya majaji watano wa Iran na mmoja wa viongozi wa kundi mashuhuri la usalama wa mtandao, kwa madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Kallas alidai kwenye X, “Wakati dunia nzima imeelekeza macho yake kwenye vita vya Mashariki ya Kati, hatupaswi kupoteza mtazamo kuhusu ukandamizaji wa Iran dhidi ya wananchi wake.”

Alidai kuwa majaji hao walihusika katika kesi dhidi ya makundi ya kidini madogo, wapinzani wa kisiasa na wanaharakati wa haki za binadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *