“Tangu 2015, idadi ya watu waliolazimika kuhama makwao kutokana na vita na mateso imeongezeka karibu mara mbili, na kufikia milioni 122,” amesema Grandi.

Amebainisha hatua muhimu za wakimbizi zaidi ya milioni moja wa Syria kurudi nyumbani, ishara ya matumaini katikati ya migogoro ya dunia.

Kuongezeka kwa upinzani dhidi ya wakimbizi

Grandi amekemea upinzani unaoongezeka dhidi ya wakimbizi katika baadhi ya sehemu duniani, akiueleza kuwa ni “umeingizwa siasa na upotoshaji, lakini haupunguzi ukweli wake.”

Amesisitiza kuwa mifumo ya hifadhi iko chini ya shinikizo la siasa za ndani na bajeti za misaada za kigeni zinazoendelea kupungua.

“Tatizo lililopo si la misingi,” amesema. “Haki ya kusaka hifadhi haikuanza miaka 75 iliyopita. Wajibu wa kimaadili wa kuwapa hifadhi wale wanaokimbia hatari umewekwa kwenye maandiko matakatifu duniani kote.”

Changamoto za uendeshaji na mgogoro wa fedha

Kamishna Mkuu huyo ameonya kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR linakabiliana na shinikizo la kifedha ambalo halijawahi kushuhudiwa.

“Kama hali ilivyo sasa, tunakadiria kuwa tutamaliza mwaka 2025 na dola bilioni 3.9 tu za fedha zilizopo,ikiwa ni pungufu ya dola bilioni 1.3 ikilinganishwa na 2024 sawa na takriban asilimia 25 chini,” amesema Grandi.

Ameeleza matokeo ya upungufu huu wa fedha, kuwa ni pamoja na kusitishwa kwa programu, kupunguzwa kwa msaada wa chakula, na kupotea kwa karibu wafanyakazi 5,000 wa UNHCR duniani.

“Karibu wafanyakazi 5,000 wa UNHCR tayari wamepoteza kazi zao mwaka huu. Hii ni zaidi ya robo ya nguvu kazi yetu yote,” amesema, akisisitiza gharama ya kibinadamu nyuma ya namba hizo.

Suluhisho za ubunifu na ujumuishaji wa wakimbizi

Licha ya changamoto hizi, Grandi ameonesha mwelekeo wa UNHCR kuelekea suluhisho endelevu na jumuishi.

“Hatuwezi tena kustahimili mfumo unaotofautisha watu waliolazimishwa kuhama makwao na wenyeji wao,” amesema.

Shirika limewekeza katika shule na kliniki za mashinani kusaidia wakimbizi na jamii zinazowakaribisha, huku likiendelea kukuza mpango wa kujitegemea kwa wakimbizi.

Ameeleza mifano kutoka Uganda, Brazil, na Colombia, ambako sera za kisasa zimewezesha watu waliotawanywa kuchangia katika uchumi wa maeneo yao.

Wajibu wa diplomasia ya kibinadamu

Grandi amesisitiza umuhimu wa kujihusisha katika maeneo ya migogoro, akiielezea kama aina ya “diplomasia ya kibinadamu.” Amebainisha kuwa Syria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, na Myanmar kama maeneo ambapo UNHCR inaendelea kurahisisha kurejea kwa amani na kuendeleza utulivu. “Lazima tukae tukijihusisha. Moja ya heshima kubwa ya kufanya kazi na UNHCR ni kudumisha mipaka kati ya misaada na diplomasia. Kusaidia wakimbizi na, kwa kufanya hivyo, kufungua milango ya amani pale amani inaonekana haiwezekani.”

Wito wa umoja na mshikamano

Akihitimisha hotuba yake, Grandi amewashukuru wafadhili, nchi zinazowakaribisha wakimbizi, na wakimbizi wenyewe.

“Shukrani maalum kwa nchi zinazowakaribisha wakimbizi kwa kubeba jukumu kubwa mlilopewa. Ninyi mmekuwa waketezi wakuu wa wakimbizi. Mimi nimejaribu kuwa mketezi wenu mkuu,” amesema.

Ameikumbusha jumuiya ya kimataifa kuwa ingawa njia mbele ni yenye changamoto, matumaini na hatua bado ni muhimu.

“Hakuna mwaka rahisi kuwa mkimbizi na kamwe hautakuwepo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *